Ticker

10/recent/ticker-posts

PROF NDALICHAKO AKERWA NA USIMAMIZI MBOVU WA MIRADI YA ELIMU, ATOA MAELEKEZO KWA KATIBU MKUU


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akikagua moja ya nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Kasumo iliyoko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akitoa maelekezo  mara baada ya kukagua ujenzi wa mabweni ya shule sekondari Muyama iliyoko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizungumza na wanafunzi katika shule ya sekondari Janda iliyopo Wilayani Buhigwe mkoani Kigoma mara baada ya kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa shuleni hapo


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameonesha kukerwa na usimamizi mbovu wa miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma na kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara anayoisimamia, Dkt. Leonard Akwilapo kuleta wataalamu watakaofanya ukaguzi maalum wa utekelezaji wa miradi ya elimu katika wilaya hiyo.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo  Wilayani Buhigwe mkoani Kigoma mara baada ya kukagua baadhi ya  miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)na kubaini uwepo wa kasoro kadhaa ikiwemo matumizi ya vifaa vya ujenzi vilivyo chini ya Kiwango na  majengo ya shule ya Msingi ya mfano Bwega  kutofautiana na ramani iliyopendekezwa na wizara .

"Kwa ujumla usimamizi wa Miradi katika wilaya ya Buhigwe  siyo mzuri, maafisa elimu hawawajibiki katika kuangalia kazi zao, unakuta kazi zimefanyika hovyo, watu hawafuatilii," alisema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe hatimizi wajibu wake ipasavyo kwa kuwa ameshindwa kusimamia miradi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa na kuruhusu matumizi ya vifaa vya ujenzi visivyo na ubora lakini pia ameshindwa kufuata ramani  katika ujenzi wa majengo ya shule ya msingi ya mfano inayojengwa wilayani humo.

Kiongozi huyo amesema tayari  amewasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Leonard Akwilapo ili ufanyike ukaguzi wa kina katika miradi ya elimu  Wilaya ya Buhigwe lengo likiwa ni kubaini mapungufu na iwapo kuna mtu kafanya uzembe kwa manufaa yake awajibike.

"Inabidi kabla ya kuleta fedha nyingine za miradi ya elimu wilayani Buhigwe ije timu ya watalaamu mainjinia wachunguze walinganishe BoQ na kilichofanyika, haiwezekani turuhusu uzembe kama huu kuendelea kwenye miradi inayotumia fedha ya wananchi wanyonge," aliongeza Waziri Ndalichako.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayanalina amemshukuru Waziri Ndalichako kwa ziara yake wilayani humo na kusema kuwa  mapungufu yote yaliyobainika tayari  Kamati yake imeyatolea maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na kwamba zoezi linaloendelea ni kuwachukulia hatua wahusika.

"Kamati ya Usalama ya wilaya ilibaini mapungufu katika miradi mbalimbali na tulitoa maelekezo kupitia kwa  Mkurugenzi na vyombo vyetu vilishaagizwa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki," amesema Mkuu wa Wilaya hiyo, Ngayalina.


Naye mMkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Anosta Nyamoga amesema ofisi yake tayari imemfukuza kazi fundi aliyekuwa na mkataba wa kufanya ukarabati na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Janda kutokana na kufanya kazi hiyo chini ya viwango na kuahidi kuzifanyia kazi kasoro zote ambazo zimebainishwa na Waziri Ndalichako.

Akiwa wilayani Buhigwe Waziri Ndalichako amekagua miradi ya elimu katika shule ya msingi Bwega, shule ya sekondari Janda,  shule ya sekondari Muyama na shule ya msingi Kasumo ambayo kwa pamoja inatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.

Waziri Ndalichako yuko Mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na Halmashauri ya Mji Kasulu.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/31hZwZJ
via

Post a Comment

0 Comments