Ticker

10/recent/ticker-posts

Ole Nasha atoa onyo kwa watakaovujisha mitihani, awapa neno Wanafunzi

Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imewaonya walimu na maafisa elimu kuacha tabia ya kuvujisha mitihani na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote wakataojaribu kuvujisha mitihani.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe William Ole Nasha wakati akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi kwenye mahafali ya kidato cha nne kwenye Shule ya Sekondari ya Kwamtoro iliyopo Wilayani Chemba mkoani Dodoma.

Ole Nasha amesema kumekuepo na tabia ya baadhi ya walimu na viongozi wanaohusika na elimu kuvujisha mitihani hasa ile ya ngazi ya Taifa jambo ambalo linaharibu taswira ya elimu nchini.

Amewataka wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne kutodanganyika kununua mitihani kutoka kwa watu wanaowalaghai kutaka kuwauzia na badala yake watoe taarifa kwenye vyombo vya sheria.

" Niwapongeze wanafunzi wote ambao leo mnaagwa, hatua hii ni kubwa sana kwenye maisha yenu. Tunajivunia nyinyi kwa kuwa ndio zao la kwanza la Elimu bure toka Mhe Rais alivyotangaza kufuta ada mashuleni mwaka 2016 ambapo nyie ndio mlikua mnaanza kidato cha kwanza.

Niwasihi msidanganyike eti mkauziwa mitihani. Hasara zake ni kubwa na zitawaponza. Tumieni elimu na maarifa ambayo walimu wenu wamewafundisha kuweza kufanya vizuri mitihani yenu, lengo ni kuona nyinyi nyote mnaogwa leo mnafaulu na kuendelea na kidato cha tano," Amesema Ole Nasha.

Amesema Wilaya ya Chemba mwaka jana ilikutwa na kashfa ya kuvujisha mitihani hivyo kuwataka kuacha tabia hiyo na watakaobainika sheria kali itachukuliwa dhidi yao.

Ole Nasha ameahidi pia kumaliza changamoto ya nyumba za walimu katika shule hiyo ambapo amesema atatoa maelekezo kwa watendaji wa Wizara yake ili Shule ya Kwamtoro iweze kupatiwa fedha za ujenzi wa nyumba hizo.

Aidha ameitaka Bodi ya Shule kuhakikisha inaharakisha ujenzi wa bweni la wasichana ili likamilike haraka ili waweze kupatiwa fedha zingine kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bweni lingine la wavulana.

" Nimefika hapa na nimekagua maendeleo ya ujenzi wa bweni la wasichana, sijaridhishwa nalo ndio maana mlivyoomba niwapatie fedha za ujenzi wa bweni la wavulana nimekataa. Hakikisheni mnamaliza hilo la kwanza ndio mje tuwapatie fedha za ujenzi wa bweni la pili.

Mhe Rais amefanya Mapinduzi makubwa kwenye sekta ya elimu zaidi ya Bilioni 945 zimetumika kwenye sera hii ya elimu bure. Ni jukumu lenu sasa wanafunzi kusoma kwa bidii ili kumpa moyo Rais wetu kwa kazi kubwa anayofanya ya kutuletea maendeleo wananchi tulio wanyonge," Amesema Mhe Ole Nasha.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amemshukuru Mhe Naibu Waziri kwa kukubalj kuhudhuria mwaliko huo na kumuahidi kuongeza usimamizi katika sekta hiyo muhimu kwenye maendeleo ya Nchi na hasa katika kudhibiti vitendo vya uvujishaji mitihani.

Nae Mbunge wa Jimbo la Chemba, Juma Nkamia amishukuru Wizara ya Elimu kwa namna ambavyo imekua ikitoa fedha katika kuhakikisha miradi ya elimu ndani ya Jimbo lake inatekelezwa.

" Mhe Naibu Waziri nakushukuru sana kwa kukubali mwaliko wetu wa kuwa mgeni rasmi. Tunakupongeza wewe na wizara unayoiongoza kwa jinsi ambavyo mmekua mstari wa mbele kutuletea maendeleo wananchi wa Chemba," Amesema Nkamia.

Awali Mhe Ole Nasha aliendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa matundu ya vyoo kwenye Shule hiyo ambapo kiasi cha Shilingi Milioni mbili zilipatikana na kuzikabidhi kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ili kukamilisha ujenzi huo na kumaliza changamoto hiyo.
 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe William Ole Nasha akikagua ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Kwamtoro wakati alipofika kwenye mahafali ya kidato cha nne.
 Mbunge wa Jimbo la Chemba, Juma Nkamia akizungumza wakati wa mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kwamtoro ambapo yeye ndie mlezi wa Shule hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe William Ole Nasha akizungumza wakati wa mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kwamtoro wilayani Chemba, Dodoma.
 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe William Ole Nasha akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya ya Chemba, walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kwamtoro wilayani humo wakati wa mahafali ya kidato cha nne ambapo Mhe Ole Nasha alikua mgeni rasmi.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2LRQ6zL
via

Post a Comment

0 Comments