Ticker

10/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI MABULA AWATULIZA WANANCHI WA KIJIJI CHA SINDENI HANDENI

Na Munir Shemweta, WANMM HANDENI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewatuliza wananchi wa kijiji cha Sindeni kilichopo Tarafa ya Sindeni wilayani Handeni mkoani Tanga kufuatia mgogoro kati yao na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuhusu mpaka baina ya kijiji cha Sindeni na Shamba la Miti la Korogwe.

Dkt Mabula aliwatuliza wananchi hao baada ya kufika katika shamba la Miti la Korogwe lililopo wilayani Handeni kukagua maendeleo ya Ujenzi wa ofisi na Nyumba za Watumishi za TFS zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akiwa katika ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Tanga.

Dkt Mabula ametaka idara ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Handeni ikisimamiwa na Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini kuhakikisha inafanya uhakiki wa mpaka kati ya TFS na kijiji cha Sindeni na kuweka alama ili kukomesha mgogoro huo unaozuka mara kwa mara.

‘Kitakachofanyika ni uhakiki wa mipaka ya kijiji chenu kinaishia wapi, TFS wanaishia wapi, NARCO wanaishia wapi, tutaheshimu mipaka na nyaraka zilizoanzisha vijiji vyenu’’ alisema dkt Mabula.

Uamuzi wa Dkt Mabula kutoa maagizo hayo unafuatia wananchi wa kijiji hicho kulalamika mbele ya Naibu Waziri kuwa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) uliongeza eneo inalomiliki katika shamba hilo kwa kuingia ndani ya eneo la kijiji cha Sindeni jambo linalochochea mgogoro kati ya pande hizo.

Ally Mhina mkazi wa kijiji cha Sindeni alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa, TFS iliacha eneo lake la asili na kuongeza eneo lingine kuingia kijiji cha Sindeni wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Kwa upande wake Meneja wa Shamba la Miti la Korogwe Pregreen Mushi alisema, wenyeji wa Sindeni walivamia eneo la Wakala wa Huduma za Misitu huku wale wa Kwamatuko na Kwaingoma wakiuza maeneo ya hifadhi kwa jamii ya wafugaji na Mkuu wa Wilaya ya Handeni alishatoa agizo wote waliovamia kuondoka eneo la hifadhi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe alisema alishashughulikia mgogoro huo na kuwataka wasioridhika wasioridhika na utatuzi wake kwenda mahakamani na kufafanua kuwa katika jitihada zake za kutafuta suluhu ya mgogoro huo baadhi ya wananchi walikubali kuwepo msitu huo na sasa wananufaika kwa kupatiwa huduma mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mustafa Beleko alisema pamoja maagizo ya Naibu Waziri kuhusiana na uhakiki wa mpaka kati ya kijiji cha Sindeni na TFS lakini wao kama halmashauri watachukua ramani ya kijiji wakati wa uhakiki mipaka ili kukomesha kuibuka kwa mgogoro huo mara kwa mara.

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliagiza pia kuweka alama za mpaka kati ya Wakala wa Huduma za Misitu na NARCO kufuatia suluhu ya mpaka kati ya taasisi hizo mbili za serikali kushindikana kutekelezwa kwa madai kuwa NARCO ilikaa kimya katika utekelezaji makubaliano ya kuchangia gharama za ubainishaji mipaka.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Shamba la Miti la Shume Lushoto mkoani Tanga linalomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu katika wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa miradi inayosimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Lushoto January Lugangika.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sindeni katika eneo la Shamba la Miti la Korogwe lililopo Handeni aliposikiliza malalamiko yao ya mpaka kati yao na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa jana usiku akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi inayofanywa na Shirika hilo katika mkoa wa Tanga. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhandisi Mawanaasha Tumbo.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2pRVz0E
via

Post a Comment

0 Comments