Ticker

10/recent/ticker-posts

MAKAMU WA PILI WA RAIS AZINDUA SERA YA VIWANDA ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akikata Utepe kuashiria Uzinduzi wa Vitabu vya Sera ya Viwanda katika hafla ya Uzinduzi wa Sera ya Viwanda 2019-2029,iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul wakil kikwajuni Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Baloz Seif Ali Idi akitoa hotuba ya Uzinduzi wa Sera ya Viwanda 2019-2029,iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul wakil kikwajuni Zanzibar.
Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali akitoa Hotuba katika hafla ya Uzinduzi wa Sera ya Viwanda 2019-2029,iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul wakil kikwajuni Zanzibar.
Muakilishi kutoka Ubalozi wa Sweden Jenny Akeback akitoa hotuba katika hafla ya Uzinduzi wa Sera ya Viwanda 2019-2029,iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul wakil kikwajuni Zanzibar.
Muakilishi kutoka UNIDO Steven Cargbo akitoa hotuba katika hafla ya Uzinduzi wa Sera ya Viwanda 2019-2029,iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul wakil kikwajuni Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Juma Hassa Reli akitoa hotuba ya Makaribisho katika hafla ya uzinduzi wa Sera ya Viwanda 2019-2029-iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul wakil Kikwajuni Zanzibar.
Baadhi ya waheshimiwa na Wageni waalikwa waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Sera ya Viwanda iliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdull wakil kikwajuni Zanzibar.PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR.

………………….

Na Khadija Khamis -Maelezo Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaomba Washirika Binafsi wa Sekta ya Viwanda pamoja na Wadau wa Maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Sera ya Viwanda Nchini ya Mwaka 2019 – 2029 ili ifikie lengo la kuifanya Zanzibar kuwa ya Viwanda.

Balozi Seif alitoa ombi hilo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Vitabu Vitano vya Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema Sera ya Viwanda ikiwa ni miongoni mwa Vitabu vilivyozinduliwa na kupata baraka zote za Serikali itachangia kuimarika kwa Sekta hiyo kwa kuzingatia utayarishaji wake imewashirikisha wadau wote wa Maendeleo ya Viwanda na kuzingatia maoni na michango iliyotolewa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Sera hiyo ni matokeo ya mapitio ya Sera ya Viwanda ya Mwaka 1998 iliyokuwa imepitwa na wakati ambayo pia inakwenda sambamba na Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 ibara ya 84 {d} inayozungumzia kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara.

Balozi Seif alisema utekelezaji wa kazi zitaimarisha mazingira bora ya Uwekezaji, uzalishaji wa bidhaa kupitia Viwanda vilivyopo ndani pamoja na kuanzisha vipya ili Taifa lifanikiwe kukabiliana na tatizo la ajira kwa Vijana, kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza uagizaji bidhaa kutoka nchi za nje.

“ Ninatambua kwamba kuitekeleza Sera ya Viwanda ni lazima kila Mshirika apate fursa ya kusoma vitabu hivyo ili aweze kutimize wajibu wake ipasavyo”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba kwa vile Sera ya Viwanda Zanzibar imeshapata baraka zote na kukubalika katika ngazi ya juu, hivyo Serikali Kuu itajitahidi kuyatekeleza na kuyasimamia kwa upande wa Sekta ya Umma.

Alielezea kuwa vitabu vilivyozinduliwa vinategemewa kuwa na mwanzo mzuri wa kukuza sekta ya Viwanda ambapo Wafanyabiashara watapata uelewa kuhusiana na mazingira ya ufanyaji wa biashara pamoja na kupata muongozo maalum utakaowasaidia wafanyabiashara na bidhaa kupitia daftari maalum.

Balozi Seif aliwahakikishia Washirika wa Sekya ya Viwanda na Biashara kwamba Serikali Kuu itazifanyia kazi changamoto zote zilizopo katika urahisishaji biashara katika maeneo ya usafirishaji na uagizaji bidhaa, usajili na uhaulishaji wa mali pamoja na upatikanaji wa vibali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizitaka Mamlaka za utoaji wa leseni na Mamlaka za usimamizi kuchukuwa hatua katika maeneo yote ambayo hayakufanya vizuri ili kurahisisha ufanyaji biashara.

Balozi Seif alisema bado ipo kazi kubwa iliyo mbele kwa Taifa ya kuwaomba Wawekezaji wengi zaidi kutumia fursa za Uwekezaji katika ujenzi wa Viwanda Vipya huku akiwataka Wananchi waendeleze amani iliyopo itakayowapatia ushawishi Wawekezaji hao.

Akitoa salamu Mwakilishi kutoka Sekta Binafsi Bwana Ahmed Yussuf alisema Kundi lao limepata faraja kubwa kutokana na ushiriki wao kwenye utayarishaji wa Vitabu hivyo muhimu kwa Maendeleo ya Sekta ya Biashara Zanzibar.

Bwana Ahmed alisema mchakato huo umeanza kwa muda kiasi, licha ya kuchelewa lakini kilichozingatiwa ni umakini wa kusonga mbele na akashauri uwepo wa ulinzi makini wa Viwanda vitakavyoanzishwa Nchini ili lile lengo lililokusudiwa likamilike vyema.

Nao kwa upande wao wakiwasilisha Salamu wa Taasisi zao, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Viwanda {UNIDO} Bwana Stephen na Mwakilishi wa Balozi wa Sweeden Nchini Tanzania Bibi Jane Akebak walisema mafanikio makubwa ya uimarishaji wa Sekta ya Viwanda utafanikiwa vyema endapo Sera za Sekta hiyo zitaimarishwa na kuwa wazi.

Wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuliona hilo kwa uamuzi wake wa kuandaa Sera, Miongozo na masuala mengine muhimu yanayojenga mazingira bora ya kuendeleza Sekta ya Viwanda sambamba kwa kushirikisha Sekta Binafsi.

Walieleza kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Viwanda {UNIDO} pamoja na Washirika wengine wataendelea kuiunga mkono Zanzibar katika Mikakati yake ya kuvifanya Visiwa vya Zanzibar kuingia katika Mfumo wa Viwanda katika uendeshaji wake wa Uchumi.

Walisema Tafiti zitafanywa zinazokwenda sambamba na Wataalamu wa Taasisi hizo kuendelea kutoa mafunzo kwa Vijana wa Zanzibar katika kuona Sekta ya Viwanda inaendelea kusonga mbele kwa kipindi kirefu ikilenga kupunguza tatizo la Ajira hasa kwa Vijana.

Walifahamisha kwamba Sekta ya Viwanda Duniani imeanza tokea Karne ya 19 kwa kujikita zaidi katika masuala ya Kilimo jambo ambalo wataalamu walipelekea kubadilisha mfumo huo na kuelekeza nguvu zaidi katika furza zaidi za ajira kwa kuanzisha uzalishaji wa biadhaa mbali mbali.

Akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua Vitabu hivyo Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali alisema uzinduzi wa Vitabu vya Sekta ya biashara umetoa mwanga kwa safari ya Zanzibar kuelekea kwenye Maendeleo ya uhakika.

Balozi Amina alisema Wizara ya Biashara itaendelea kubeba dhima ya kuiona Zanzibar inastawi na kufanikiwa katika mwenendo mzima wa Sekta ya Biashara inayotowa fursa kubwa katika utoaji wa ajira miongoni mwa Wananchi walio wengi.

Wajasiri amali wadogo wadogo wamezingatiwa katika mfumo wa Miongozo ya Sera na Vitabu hivyo watakaokuwa na fursa pana zaidi ya kujengewa mazingira mazuri wa bidhaa zao zitakazokuwa na muelekeo wa kuuzwa katika Masoko ya Kimataifa likiwemo lile la AGOA.

Waziri wa Biashara na Viwanda ameushiriki Uongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa unaoshughulika Viwanda {UNIDO} na Ubalozi wa Sweeden Nchini Tanzania kwa michango yao iliyofanikisha kukamilika kwa Vitabu hivyo.

Jumla ya Vitabu Vitano vimezinduliwa kuhusiana na Sera ya Viwanda, Ripoti ya tathmini ya mazingira ya ufanyaji wa biashara, Daftari la Wafanyabiashara, Muongozo wa usafirishaji na uagizaji pamoja na Taarifa za Wazalishaji wa Kazi za Mikono Zanzibar zinazotarajiwa kuuzwa katika Soko la AGOA.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/33XPqij
via

Post a Comment

0 Comments