Ticker

10/recent/ticker-posts

KASI YA WAKANDARASI MIRADI YA UMEME VIJIJINI TANGA YAIRIDHISHA BODI

Na Veronica Simba – Tanga
Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB) imekiri kuridhishwa na kasi ya utendaji kazi wa wakandarasi Derm Electrics (T) Ltd na JV Radi Services Ltd, Njarita Contractors Ltd & Aguila Contractors Ltd; wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo, Oktoba 23, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi hiyo, Mhandisi Styden Rwebangila alisema wakandarasi hao wanafanya kazi nzuri kwani mpaka sasa wamevuka asilimia ya utekelezaji waliyopaswa kuwa wamefikia.

“Mkandarasi Derm Electrics amefikia asilimia 83.5 kati ya 66 aliyopaswa kuwa amefikia wakati mwenzake akiwa amefikia asilimia 67 kati ya 66 aliyopaswa kuwa amefikia,” alibainisha Mwenyekiti.

Akifafanua, Mhandisi Rwebangila alisema Kamati yake imefarijika kuona mabadiliko makubwa aliyofanya Mkandarasi huyo wa pili (JV), kwani awali alikuwa akisuasua kiasi cha kuwa kwenye hatari ya kufutiwa mkataba wake.

“Kwa niaba ya Bodi, tumeridhishwa na utendaji wa wakandarasi katika Mkoa wa Tanga.”

Hata hivyo, Mhandisi Rwebangila alisema katika ziara ambayo Kamati yake imefanya mkoani humo kwa muda wa siku mbili, imebaini changamoto kadhaa ikiwemo wakandarasi kutokugawa vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wenye uhitaji kama serikali ilivyowaelekeza.

Kufuatia changamoto hiyo, alisema, Kamati yake imetoa maelekezo kwa Mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Mkoa na Wilaya, waweke mkakati utakaohakikisha vifaa hivyo vinafungwa kwa wananchi husika kama ilivyoelekezwa.

Aidha, alitaja changamoto nyingine kuwa ni uhaba wa nyaya za umeme suala ambalo alisema limekwishafikishwa kwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ambaye naye amechukua hatua kwa kupanga kukutana na wazalishaji wote wa nyaya nchini Oktoba 29 mwaka huu, ili kujua tatizo linalosababisha kutopatikana kwa nyaya hizo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu, ambaye amefuatana na Bodi husika katika ziara hiyo, alitoa wito kwa wakandarasi kuhakikisha wanapeleka nguzo zote maeneo ya kazi na kuzisimika ili kuepuka changamoto ya kukwama kutekeleza hilo kutokana na kipindi cha mvua kinachoendelea ambacho mara nyingi huharibu miundombinu ya barabara.

Pia, aliwataka wakandarasi kuwaunganishia umeme wateja wote waliopo ndani ya wigo pasipo kisingizio cha mteja kutotandaza mfumo wa nyaya (wiring) kwenye jengo lake kwani kuna kifaa cha UMETA kinachofaa kwa wateja wa aina hiyo.

“Natamani wakandarasi watuambie wamegawa vifaa vyote 250 ambavyo kila mmoja kapewa kwa kila eneo ili sisi tuwaongezee vingine badala ya kukaa navyo tu pasipo kuwafungia wananchi,” alisema Olotu.

Awali, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Sebastian Masanja, alitoa pongezi kwa Rais John Magufuli na Serikali kwa ujumla, hususan Wizara ya Nishati, kwa kutekeleza mkakati wa kupeleka umeme vijijini.

Alisema, umeme vijijini umekuwa ni mkombozi kwa vijana ambao hawakuwa na kazi na kuzurura hovyo. “Sasa wengi wamejiajiri katika shughuli mbalimbali ikiwemo saluni na kuchomelea vyuma na wanajipatia kipato kuendesha maisha yao na familia zao.”

Wakandarasi wote wameahidi kukamilisha kazi kwa viwango stahiki na kwa wakati kama serikali ilivyoagiza, yaani Desemba 31, mwaka huu.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Styden Rwebangila akizungumza, wakati Kamati hiyo ilipokutana na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga (hawapo pichani), Oktoba 23, 2019.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Styden Rwebangila (meza kuu – katikati), akiongoza kikao baina ya Kamati hiyo na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga, Oktoba 23, 2019.
 Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), Louis Accaro, akifuatilia kikao baina ya Kamati hiyo na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga (hawapo pichani), Oktoba 23, 2019.
  Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu, akizungumza wakati Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), ilipokutana na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga (hawapo pichani), Oktoba 23, 2019.
 Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuyuni, wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, Zihirwani Mbwambo (kushoto), akizungumzia hali ya upatikanaji umeme kijijini hapo alipotembelewa na Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), ofisini kwake, Oktoba 23, 2019.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Styden Rwebangila (katikati) na Ujumbe wake, wakiwa katika kikao cha ndani na mameneja wa TANESCO mkoani Tanga pamoja na wakandarasi wanaotekeleza miradi husika mkoani humo, walipokuwa katika ziara ya kazi, Oktoba 23, 2019.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/33YT6jQ
via

Post a Comment

0 Comments