Ticker

10/recent/ticker-posts

JOPO LA MAJAJI WATATU KUSIKILIZA MAOMBI YA RUFAA

Na Magreth Kinabo-Mahakama

Mahakama ya Rufani Tanzania, imesema kwamba shauri la maombi jinai la mapitio ya nyongeza ya muda, haliwezi kuendelea kusikilizwa kwa sababu linahitaji na jopo la majaji watatu.

Uamuzi huo ulitolewa leo, Oktoba 15, mwaka huu na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Rehema Kerefu wakati akisikiliza shauri la maombi ya jinai ya mapitio ya muda linalomkabili Job Mlama na wenzake wawili, dhidi ya Jamhuri,ambayo iliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidambo wote wakiwa mkoani mwanza kwa njia ‘Video conference’.

Shauri hilo liliendeshwa huku wakili huyo na wahusika, wakiwa mkoani Mwanza, na Jaji Kerefu katika Kituo cha Habari na Mafunzo kilichopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Katika shauri hilo, mleta maombi hayo, Mlama aliomba mahakama hiyo isikilize maombi ya mapito ya nyongeza ya muda kwa njia ya ‘Video Conference’.

Jaji Kerefu alitoa uamuzi huo, baada ya kuuliza upande wa Jamhuri kuwa uko tayari kuendelea na maombi hayo ya mapitio ya muda, ambapo ulikubali, ndipo alipotoa uamuzi huo, wa shauri kuwa linapaswa kusikilizwa na jopo la majaji watatu kama sheria inavyosema.

Katika shauri lingine la maombi ya jinai ya mapitio ya nyongeza ya muda linalomkabili, Weisiko Ruchere dhidi ya Jamhuri, ambaye aliwakilishwa na wakili Geofrey Kanje na kusikilizwa na Jaji Kerefu.

Wakili Kanje aliomba mahakama hiyo iongeze muda wa maombi hayo kwa sababu ya mleta maombi kutokuwa na msaada wa kisheria.

Akijibu hoja hiyo Wakili wa Serikali Mwandamizi,Anjelina Nchalla alisema hakuna sababu za msingi alizozitoa mleta maombi zilizosababisha achelewe kuleta maombi hayo kwa kuwa ni mwaka moja na nusu tangu yalipotupiliwa mbali Novemba 29, mwaka 2017.

Akisikiliza maombi hayo Jaji Kerefu alisema atatoa uamuzi na wahusika watataarifiwa baadaye.

Shauri lingine lililosikilizwa na Mhe. Jaji Ignas Kitusi, ambapo mleta maombi ya jinai ya mapitio ya nyongeza ya muda, Reuben Juma dhidi ya Jamhuri iliyowakilishwa na Wakili wa Serikali Maryyasintha Lazaro na Wakili wa serikali Mwanahawa Shangale, ambao walipinga ombi hilo.

Katika shauri hilo, Juma aliomba mahakama hiyo isitilie maanani pingamizi la mawakili hao kwa sababu limekuja nje ya muda na pia alikosa msaada wa kisheria wa kuwasilisha ombi lake, ndani ya wakati. 

Huku Wakili huyo Mwandamizi aliomba mahakama hiyo itupilie mbali maombi hayo kwa kuwa kukosa msaada wa kisheria sio sababu ya msingi na maombi hayo hajazingatia matakwa ya kisheria.

Akijibu hoja ya Wakili huyo Mwandamizi, Jaji Kitusi alisema ni takwa la kisheria la mleta maombi.

Akisikiliza hoja hizo,Jaji Kitusi alisema ataenda kuandaa uamuzi na wahusika watataarifiwa baadaye.

Shauri lingne la madai lililosikilizwa na Jaji huyo, la mleta maombi ya nyongeza ya muda ambaye ni Geita Gold Mine Limited, aliyewakilishwa na Wakili Faustine Mwalongo dhidi ya Truway Muneth na wenzake waliowasilishwa na wakili Mwita Emmanuel, ambaye aliomba mahakama isikubali maombi hayo kwa sababu yalikuwa nje ya muda na yalipaswa kuandaliwa ndani ya siku moja.

Wakati Mwalongo aliomba maombi hayo yakubaliwe na mahakama hiyo kwa kuwa yako ndani ya muda wa siku tatu, yakiwa yanaandaliwa na kuwasilishwa mahakamani, hivyo hakuna nyaraka inayosema maombi yaandaliwe ndani ya siku moja.

Katika hatua nyingine Jaji mwingine wa mahakama hiyo, Mhe. Dkt. Mary Levira alihairisha shauri la maombi ya nyongeza ya muda la Mugeta Manyama dhidi ya Jamhuri kwa sababu mleta maombi haifahamiki yuko gereza gani.

Aidha Dkt. Levira pia alisikiliza shauri la maombi ya mapitio ya nyongeza ya muda la Kafuba Mwangulindi dhidi ya Jamhuri na litatolewa maamuzi baadaye.

Kwa upande wa mkoa wa Bukoba Mahakama hiyo imesikiliza mashauri sita kwa njia hiyo pia, ambapo mashauri matano ni ya maombi ya jinai ya nyongeza ya muda na moja la maombi ya madai ya nyongeza ya muda. Mashauri hayo yalisikilizwa na majaji watatu ambapo kila mmoja alisikiliza mashauri mawili.

Majaji waliosikiliza mashauri hayo ni Mhe. Winfrida Korosso, Mhe. Barke Sehel na Mhe. Lugano Mwandambo. Mashauri hayo baadhi yamesikilizwa na kumalizika, mengine maamuzi yatatolewa baadaye.

Mahakama hiyo itaendelea na mashauri mengine maombi ya jinai na madai kesho, Oktoba 16 kwa njia ya ‘Video Conference’ yaliyoko masjala ya Mbeya na Mwanza.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2IV3K2Z
via

Post a Comment

0 Comments