DC Katambi atoa siku tatu kwa mkandarasi aliejenga ukuta chini ya kiwango

  Masama Blog      
Charles James, Michuzi TV
KUFUATIA kutoridhishwa na uzio wa ujenzi wa mradi wa upanuzi uzalishaji wa umeme jijini Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi ameagiza kuvunjwa kwa ukuta huo kutokana na kujengwa chini ya kiwango.

DC Katambi ametoa siku tatu kwa mkandarasi huyo kutoka Kampuni ya KEC ya nchini India kuvunja uzio wa ujenzi huo unaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 125.

Maagizo hayo ameyatoa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza ya kutembelea ujenzi wa mradi huo unaojengwa kwa fedha za Serikali.

Amesema matofali yaliyotumika kujenga mradi huo hayana ubora unaotakiwa hali iliyopelekea kubomoka na hata yanapondoshwa huvunjika kutokana na kukosa viwango.

“ Ukitazama matofali haya yaliyotumika kujenga uzio huu hayana ubora kutokana na kubomoka, hata ukiyashika kwa mkono tuu bila kutumia vipimo vyovyote hali hii hatuwezi kuifumbia macho ni lazima ukuta huu uvunjwe na makandarasi kwa gharama zake mwenyewe.

Fedha hizi ni za walipa kodi wa Kitanzania hatuwezi kukubali watu wachache waichafue Serikali yetu ambayo inafanya kazi usiku na mchana kuwaletea maendeleo wananchi wetu. Ndio maana nimetoa siku tatu ukuta uvunjwe na ujengwe tena, " Amesema DC Katambi

Amesema ukuta huo sio tu umejengwa chini ya kiwango lakini pia umekiuka masharti na miongozo ya mkataba wa awali kama ambavyo BOQ inaelekeza.

“Hapa leo nakuja wapo wenyewe hakuna mtu hata mmoja wa Tanesco, sasa hali hii inatishia sana kwani mradi huu unaweza kuchakachukiwa kwa kiwango kikubwa sana na fedha za watanzania zikaliwa bila kuwepo na tija yeyote” Amesema Katambi.

Kwa upande wake mhandisi Shafii Kiula, kutoka shirika la ugavi wa umeme nchini Tanesco alimesema shirika hilo tayari lilishamwandikia barua mkandarasi wa mradi huo kuuvunja ukuta kwa gharama zake na kuanza upya ujenzi kutokana na matofali yaliyotumika kukosa ubora.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2otc3M4
via
logoblog

Thanks for reading DC Katambi atoa siku tatu kwa mkandarasi aliejenga ukuta chini ya kiwango

Previous
« Prev Post