Ticker

10/recent/ticker-posts

BILIONI 10 ZATENGWA KWA AJILI YA UJENZI WA CHUO CHA UFUNDI CHATO

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akicheza muziki na baadhi ya viongozi wa Chato wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na wadau wa elimu(hawapo pichani) waliohudhuria sherehe za  uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Chato


Wizara ya Elimu, Sayansi na  Teknolojia imetenga jumla ya Shilingi bilioni 10.7 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa chuo hicho, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema ujenzi wa chuo huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.

"Nawapongeza viongozi wa Halmashauri ya Chato kwa usimamizi mzuri kwani mpaka sasa mradi huu umefikia asilimia 78 huku mkandarasi akiwa ameshalipwa asilimia 41 ya pesa yote  jambo linaloonyesha kwamba kuna fedha itabaki ambayo itasaidia kuongeza majengo mengine," amesema Waziri Ndalichako.

Aidha, Waziri Ndalichako amewataka Wakandarasi na Washauri Elekezi wanaofanya kazi za Wizara ya Elimu kuwa wazalendo na kuacha kuongeza gharama za miradi inayotekelezwa na wizara hiyo.

"Tumegundua katika mikataba mingi malipo ya washauri elekezi yanalipwa kulingana na kiwango anacholipwa mkandarasi hivyo kufanya mkandarasi  kuongeza gharama na kutokukagua vizuri miradi hiyo," ameelezea Profesa Ndalichako.

Waziri huyo amesema Wizara inafanya mapitio hata kwa miradi iliyoishakamilika  ili kujiridhisha na gharama halisi za utekelezaji na kuwezesha kutoa fedha zinazolingana na gharama na kuhakikisha miradi inakamika kwa viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema ujenzi wa chuo hicho cha kipekee mkoani humo ni mwendelezo wa mageuzi makubwa yanayoshuhudiwa katika sekta ya elimu kwa kipindi cha uongozi wa serikali ya Awamu ya Tano.

"Chuo cha VETA Chato kitakuwa cha kwanza chenye ubora wa juu katika kanda ya ziwa kwa kuwa ni kikubwa  na kitakuwa na  karakana zenye vifaa vya kisasa ambavyo vitawezesha vijana wa Chato kuwa na ujuzi na maarifa," amesisitiza Mhandisi Gabriel.

Aidha, Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ameishukuru serikaki kwa kujenga chuo hicho na kuahidi kuhakikisha anahamasisha vijana wa Chato kujiunga katika chuo hicho ili kupata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi kupitia viwanda.

Kalemani amemuomba mkandarasi wa mradi huo kuongeza vijana wa Chato katika mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati kama ilivyopangwa na hatimaye mafunzo yaanze kutolewa Januari 2020.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu amesema mradi wa ujenzi chuo hicho ni miongoni mwa miradi 40 ya ujenzi wa vyuo vipya vya ufundi stadi pamoja na upanuzi wa vyuo vilivyopo lengo likiwa ni kutimiza azma ya serikali ya kuongeza upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi na hatimaye kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 200,000 ya mwaka 2016/17 hadi 700,000 ifikapo mwaka 2020.

"Mradi huu na mingine kama hii inayotekelezwa nchini inachangia utekelezaji wa azma ya serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha kuwa vijana wanapata ujuzi stahiki utakaowawezesha kuajiriwa  au kujiajiri ili kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa viwanda," amesisitiza Bujulu.

Akitoa taarifa ya Mradi huo Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya ziwa, Michael Ikongoli amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo 27 ambayo ni pamoja na madarasa, karakana, nyumba 4 za walimu, bwalo la chakula, jengo la utawala na kwamba samani zote za Chuo hicho zitatengenezwa na Chuo cha VETA Mwanza kwa gharama ya shilingi milioni 693.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2PhTshu
via

Post a Comment

0 Comments