Ticker

10/recent/ticker-posts

BENKI YA DUNIA YAIKOPESHA SERIKALI MKOPO WENYE MASHARTI NAFUU KUKABILIANA NA UMASKINI NCHINI.

Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia zimetiliana saini mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Kimarekani milioni 450 kugharamia sehemu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF.Mkataba huo umetiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James kwa niaba ya serikali na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird.

Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango amesema kupatikana kwa fedha hizo ni kiashirio kingine cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dr. John Magufuli ilivyokusudia kuweka mazingira wezeshi ya kuondoa kero ya umaskini kwa wananchi wake.

Amesema Mkopo huo wenye masharti nafuu utaelekezwa zaidi katika kusaidia jitihada za Serikali za kutatua kero ya umaskini nchini kote kwa kuwashirikisha wananchi ambao ni walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wenye uwezo wa kufanyakazi kushiriki kwenye miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao na kisha kulipwa ujira kama njia mojawapo ya kuwaongezea kipato.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird amesema Tanzania imekuwa mfano bora katika kuhudumia wananchi wanaokabiliwa na umaskini mkubwa kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii jambo ambalo limeifanya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo ya Dunia kuridhia kiasi hicho kikubwa cha fedha kutolewa kwa utaratibu wa Mkopo wenye masharti nafuu .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Taifa ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF- Dr. Moses Kusiluka ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na TASAF katika kusaidia jitihada za kupunguza umaskini nchini.

Amesema kupatikana kwa fedha hizo kutasaidia kuwafikia wananchi wenye uhitaji mkubwa nchini kote na kuwa kichocheo cha kuharakisha maendeleo na hatimaye kuliwezesha taifa kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa na kuboresha miundombinu katika sekta za elimu, afya maji huku mkazo mkubwa ukiwekwa katika kukuza uchumi wa kaya za walengwa.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga ameishukuru serikali kwa uamuzi wa kuendelea kutekeleza Mpango wa kunusuru Kaya Maskini na kuahidi kusimamia kwa uaminifu raslimali fedha ili ziweze kunufaisha taifa kupitia Walengwa.

Amesema uzoefu uliopatikana katika sehemu ya kwanza ya Mpango umeonyesha kuwa Walengwa wengi wamebadili maisha yao kwa kutumia fursa zinazotolewa na Mpango huku akitaja sekta za elimu, afya na uzalishaji mali kuwa zimechangia kwa kiwango kikubwa kuboresha maisha ya Walengwa.

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na wawakilishi wa mashirika yanayochangia fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za serikli kupita Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF. Utekelezaji wa sehemu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya maskini unatarajiwa kuanza wakati wowote baada ya kuzinduliwa rasmi na utahudumia takribani Kaya milioni 1.3.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dotto James (kushoto) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird (kulia) wakitia saini mkataba wa kuipatia Tanzania Mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia kutekeleza sehemu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitiaTASAF. 



Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Ikulu Dr. Moses Kusiluka (katikati) akizungumza mara baada ya kutiwa saini ya mkopo wenye masharti nafuu kati ya serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia ,fedha zitakazotumika kutekeleza sehemu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unatekelezwa na serikali kupitian TASAF.Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bw. Dotto James na kushoto kwake ni Mkurugenzi Makazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird (katikati) akizungumza baada ya kutia saini mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa kamati ya taifa ya Uongozi ya TASAF ,Dr. Moses Kusiluka na kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bw. Dotto James.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyevaa miwani) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) baada ya serikali kutia saini mkataba wa mkopo wenye masharti nafukutoka Benki ya Dunia, fedha zitakazotumika kutekeleza mradi wa kupunguza umaskini nchini .  


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2AQhh7w
via

Post a Comment

0 Comments