Wizara ya Afya yaingia makubaliano na Shirika la GIZ kuboresha sekta hiyo nchini

  Masama Blog      
Charles James, Michuzi TV

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeingia makubaliano na Shirika la GIZ kutoka nchini Ujerumani yenye lengo la kuboresha sekta ya Afya nchini.

Makubaliano hayo yamekwenda sambamba na kutiliana saini kwa mkataba wa kufanya kazi pamoja kwa miaka mitatu utakaogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 26.

Akizungumza baada ya kutiliana saini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk Zainab Chaula amelishukuru Shirika la GIZ kwa namna ambavyo limekua likijitoa katika kusaidia ukuaji wa sekta hiyo muhimu.

" Kwa kweli niwashukuru sana wenzetu wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani kwa namna ambavyo wamekua bega kwa bega na sisi, zaidi niwapongeze na kuwashukuru ndugu zetu wa GIZ hawa wamekua wadau wakubwa wa Afya nchini.

" Tunawaahidi kuwapa ushirikiano na kusimamia kwa ukamilifu yale yote tuliyokubaliana kuyatekeleza, lengo letu sote ni kuona sekta hii ya afya inakua na inawanufaisha Watanzania ambao ndio haswa walioipa dhamana Serikali ya awamu ya tano kuwatumikia," Amesema Dk Chaula.

Aidha amelipongeza Shirika hilo kwa kukubali kuwapatia fedha hizo kwa wakati mmoja ili iwe rahisi kuweza kutekeleza maazimio yote kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

" Ndugu zangu kazi ya Serikali ni kuwaletea wananchi wake Maendeleo na Rais wetu Dk John Magufuli ni mtu wa vitendo haswa, amedhamiria kuifanya Nchi yetu kuwa imara katika kila nyanja na afya ikiwemo, haya yote tunayoyafanya leo ni matokeo ya juhudi kubwa ambazo yeye kama Kiongozi wetu wa Nchi amekua nazo," Amesema Dk Chaula.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkazi wa Shirika la GIZ, Dk Mike Falken amesema makubaliano waliyoyafikia na Wizara ya Afya ni matokeo ya utendaji kazi wa Serikali ya Tanzania katika kuwatumikia wananchi wake.

Amesema mkataba huo umejikita katika afya ya msingi hasa katika zahanati na vituo vya afya na utalenga maeneo matano ambayo ni Uboreshaji wa Taarifa, Mama na Mtoto, Bima, Uzazi wa Mpango na Utawala Bora.

" Sisi tunawaahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati yetu, sisi tunaridhishwa na kasi ya Rais Magufuli katika kuwatumikia Watanzania na ni wazi tunamuunga mkono kwa vitendo," amesema Dk Falken.

Awali Shirika hilo lilikabidhi kwa Serikali kupitia Wizara ya Maji mradi wa Maji katika eneo la Ng'ong'onha jijini Dodoma ambao umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 331 na utahudumia wananchi takribani 12000.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Zainab Chaula (kushoto) akitiliana saini na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la GIZ, Dk Mike Falken katika hafla ya makubaliano ya Uboreshaji afya nchini
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Zainab Chaula akizungumza na viongozi wa Wizara yake pamoja na viongozi kutoka Shirika la GIZ LA Nchini Ujerumani katika hafla ya kutiliana saini makubaliano ya Uboreshaji sekta ya afya.from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2A9sKik
via
logoblog

Thanks for reading Wizara ya Afya yaingia makubaliano na Shirika la GIZ kuboresha sekta hiyo nchini

Previous
« Prev Post