Ticker

10/recent/ticker-posts

WATUMISHI WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA WATAKIWA KUTAMBUA,KUKUBALI MFUMO WA UTENDAJI WA JESHI USU

Na Ripota Wetu, Morogoro

WATUMISHI wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wametakiwa kutambua na kukubali mfumo wa utendaji wa Jeshi Usu ili kukabiliana na changamoto za uhifadhi nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy alipokuwa akifunga kikao cha pili cha bodi hiyo kilichofanyika mkoani hapa.

Amesema mabadiliko ya mfumo wa utendaji kutoka ule wa kiraia kwenda katika mfumo wa Jeshi Usu yanalenga kuleta suluhisho la kudumu katika kukabiliana na changamoto za usimamizi wa rasilimali misitu na nyuki nchini.

Mkeremy amesema kuna tofauti kubwa sana ya kiutendaji na hata matokeo katika mfumo wa kiraia na ule wa Jeshi Usu, na kwa hali ilivyo sasa mfumo wa Jeshi uso ndio mfumo pekee utakakwenda kunusuru misitu nchini.

“Niwapongeze TFS kwa kazi kubwa mnayoifanya licha ya changamoto nyingi mnazokabiliana nazo kiutendaji, changamoto hizi sasa zinakwenda kuisha, kinachotakiwa ni nyinyi watendaji sasa kutambua na kukubali mabadiliko ya mfumo wa utendaji kutoka ule wa kiraia na kwenda kwenye mfumo wa Jeshi Usu,

“kwa bahati nzuri mimi nimefanya kazi katika mifumo yote miwili nachoweza kuwaeleza ni kwamba mnaweza msione matokeo sasa lakini with time mtaona, duniani kote majeshi ya uhifadhi yanaheshimika, hakutakuwa na mwenye uthubutu wakuingia kwenye hifadhi za misitu, kila mtu anajua nini maana ya jeshi,” amesema Brigedia Jenerali Mkeremy.

Kwa Brigedia Jenerali Mkeremy ni kikao chake cha kwanza kwa mwaka 2019/2020 na cha pili tangu Bodi izunduliwe mwezi Machi mwaka huu.

Wakati huo huo Kamishna Mhifadhi Misitu nchini, Professa Dos santos Silayo amesema zaidi ya watumishi 500 wamekwishapata mafunzo ya Jeshi Usu katika chuo cha Kijeshi Mlele na Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Pansiansi na bado zoezi linaendelea.

Amesema tangu zoezi hilo la mabadiliko hayo ya mfumo wa utendaji lianze, baadhi ya maeneo yaliokuwa yana uharibifu mkubwa wa misitu yameanza kuwa salama kutokana na watendaji wake kufanya kazi kwa kuzingatia muda na taratibu.

Wajumbe wa Bodi walipata fursa ya kupanda miti katika maeneo ya Kituo cha Mbegu za Miti mkoani Morogoro kama sehemu ya kuhimiza uhifadhi kwa kupanda miti.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy  akipanda mti huku akishuhudiwa na baadhi ya wajumbe wa bodi na menejimenti ya TFS
 Kamishina Mhifadhi Misitu Profesa Dos Santos Silayo akipanda mti
 Mmoja ya wajumbe wa bodi ya ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania akipanda mti
Wajumbe wa bodi wakiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya TFS mara baada ya kumaliza kikao cha pili cha podi hiyo tangu kuzinduliwa katika ukumbi wa Kituo cha Mbegu za Misitu Morogoro jana.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2ZPjhXS
via

Post a Comment

0 Comments