Ticker

10/recent/ticker-posts

TUNAHITAJI WAWEKEZAJI KWENYE KILIMO CHA MIWA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez ambapo amewakaribisha Wacuba waje wawekeze kwenye sekta ya kilimo, hususan cha miwa.

Amekutana na kiongozi huyo leo (Jumatatu, Septemba 9, 2019) ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. Waziri Mkuu ameishukuruSerikali ya Cuba kwa ushirikiano mzuri inaoutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kuboresha maendeleo ya jamii.

“Tanzania na Cuba zina uhusiano wa kihistoria. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, yaliyokuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Cuba, hayati Fidel Castro.”

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Cuba imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa sukari, hivyo amewakaribisha Wacuba waje nchini washirikiane na Serikali ya Tanzania katika kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kuboresha kilimo cha miwa na kuanzisha viwanda vya sukari.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati yake na Serikali ya Cuba kwa kuwa nchi hiyo ni mojawapo kati ya nchi zenye ushirikano wa muda mrefu na Tanzania katika masuala ya kisiasa, kijamii, kiafya na kiuchumi.

”Mfano katika sekta ya afya, madaktari wengi kutoka Cuba wamekuwa wakija Tanzania kutibu wagonja waliokuwa na maradhi makubwa na pia Serikali ya Cuba imekuwa ikitoa fursa kwa Watanzania kwenda kusomea fani ya udaktari.”

Pia Waziri Mkuu amewakaribisha Wacuba waje wawekeze katika sekta ya utalii hususani wa fukwe kwa sababu Tanzania ina fukwe nzuri. Amesema mji mmoja wa Varadero wa nchini Cuba unaingiza watalii zaidi ya milioni moja kwa mwaka na unategemea kivutio kikubwa kimoja tu cha fukwe ambayo ina urefu wa kilomita 22.

Akizungumzia kuhusu ofisi ya ubalozi wa Tanzania zilizofunguliwa nchini Cuba, Waziri Mkuu amesema zimesaidia kurahisisha mawasiliano kwa sababu awali kulikuwa na balozi mmoja tu ambaye alikuwa akiwakilisha nchi ya Cuba nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez alisema Serikali ya Cuba itahakikisha uhusiano wake na Serikali ya Tanzania unakuwa endelevu. Pia alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.

Kadhalika kiongozi huyo amesema Serikali ya Cuba imefurahisha na kitendo cha Serikali ya Tanzania kufungua ofisi ya ubalozi nchini Cuba kwa sababu imezidi kuimarisha mahusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili. Kiongozi huyo pia amefanya ziara Zanzibar kabla ya kuja Dodoma. 
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na ujumbe kutoka nchini Cuba, ukiongozwa na Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez, kwenye ukumbi wa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Septemba 9.2019.
  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimkabidhi zawadi ya kinyago, Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez, kwenye ukumbi wa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Septemba 9.2019.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akipokea zawadi ya kitabu cha Rais wa kwanza wa Cuba, Fidel Castro, kutoka kwa Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez, kwenye ukumbi wa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Septemba 9.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez, kwenye ukumbi wa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Septemba 9.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).



from MICHUZI BLOG https://ift.tt/300g7AA
via

Post a Comment

0 Comments