Kwa Simu Toka London - NASSOR MAHRUKI: MTANZANIA PEKEE KATIKA MASHINDANO YA KIMATAIFA YA KUZUNGUKA DUNIA KWA MASHUA ZA UPEPO

  Masama Blog      
 Picha na Habari za Freddy Macha, London 
 Wangapi tumewahi kusikia mashindano ya kimataifa ya mashua za upepo (“clipper race” )? Mimi sikuyajua hadi nilipomhoji Nassoro Mahruki, Mzanzibari mshiriki wa tukio hilo litakalochukua miezi kumi na moja hadi Agosti 2020. 
Nassoro Mahruki ambaye huendesha shughuli zake za biashara za utalii visiwani Pemba na Unguja, ni Mwafrika Mashariki pekee na anasema alijitayarisha kwa miaka miwili kushiriki. “Yakubidi ufanye mafunzo na kufaulu ...” alisema akinionyesha mashua iitwayo “Zhuhai” ikiongozwa na nahodha Nick Leggatt. Zhuhai ni kati ya vyombo vingine kumi na moja vyenye majina kama “Korea”, “Punta Del Este”, “WTC Logistics”, nk.

Dimba hili lilianzishwa hapa London mwaka 1996. Mwasisi wake, aliyeshatunukiwa heshima ya “Sir” na Malkia Elisabeth wa Uingereza ni Robin Knox Johnson. Bw Johnson alikuwa mwanadamu wa kwanza kuzunguka dunia nzima kwa mashua inayotegemea upepo tu mwaka 1968. Keshafundisha zaidi ya mabaharia 5,000. Kitatange hiki kinahusu kila aina ya changamoto za kimichezo. Kushirikiana na wenzako, dhoruba zenye pepo kali, mvua, barafu, mawimbi nk. Usafiri ulioanzia London Septemba Mosi , 2019 utapitia mabara yote na bahari kubwa zaidi ya sita, Ureno, Uruguay, Afrika Kusini, Australia, China, Marekani, visiwa vya Bermuda, Panama, nk. Watarejea London Agosti 2020. Nilipowasiliana naye leo alikuwa tayari salama Ureno. Nassoro Mahruki aliyevalia bendera za Tanzania, Zanzibar, Pemba alisema mbali ya kupenda michezo ya majini lengo ni kujenga tasnia ya utalii wa majini Tanzania. “Ikiwa washindani wenzangu wako radhi kununua meli ya paundi milioni kumi, hawatashindwa kuja Tanzania kuchezea maji na kutumia dola elfu mbili kwa juma. Ni hela nzuri sana kwa utalii wetu.” Mataifa zaidu ya 40 yamo mwaka huu na Afrika ina nchi nne tu : Tanzania, Nigeria, Misri na Morocco. Tumpe heko na kumwombea dua arejee salama. Fahari yetu. 1.  
Nassoro Mahruki akiwa kazini katika mashua ya Zhuhai yenye mabaharia toka mataifa China, Marekani, Uingereza, Canada, Ufaransa, nk 2.  
Nassoro Mahruki akizungumza kando ya bandari ya Katherine Docks, London, kabla ya kusafiri na mabaharia wenzake Septemba Mosi, 2019. 3.  
Moja ya majengo ya mandhari ya hoteli Mnarani , Nungwi kaskazini ya Zanzibar. Bw Mahruki ameendesha biashara za utalii, Zanzibar na Pemba kwa miaka 23 sasa. Ni mtu anayependa kazi na shughuli azifanyazo. Mchapa kazi na Mjasiria Mali wa mfano. 4. Maelfu ya wakazi wa London waliokuja kushangilia kuondoka kwa washindani wa tukio, la Clipper Race, Jumapili Mosi Septemba, 2019 5.  
Nassoro Mahruki akiwa na nahodha wa mashua husika (“Zhuhai”), Nick Leggatt, mzawa wa Afrika Kusini mwenye uzoefu wa muda mrefu. Keshazunguka dunia kwa mashua hizi mara tatu! 7.  
Mwandishi Freddy Macha nikiwa na Nassoro Mahruki mwenye umri wa miaka 51. Mahruki alijilipia mwenyewe. Washikiri wa mataifa mengine hupata wafadhili wa kibiashara kirahisi ukilinganisha nasi Afrika Mashariki Tazama mahojiano na Nassoro Mahruki - “Kwa Simu Toka London” ( KSTL)


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/30i6NZf
via
logoblog

Thanks for reading Kwa Simu Toka London - NASSOR MAHRUKI: MTANZANIA PEKEE KATIKA MASHINDANO YA KIMATAIFA YA KUZUNGUKA DUNIA KWA MASHUA ZA UPEPO

Previous
« Prev Post