Ticker

10/recent/ticker-posts

KUMBUKIZI YA MPIGA DRUM BORA NCHINI MAREHEMU ABUU SEMHANDO BABA DIANA"

Abuu Semhando (ua jekundu mfukoni kati) akiwa Orchestra Vijana jazz Wana-Pambamoto wakiwa .Morogoro siku Mandela alipotembelea baada ya kufunguliwa. Waliokaa mbele kushoto Mpenzi, Baker Semhando (Bassist), Juma Choka (Drummer) sasa yuko Sikinde, Waliosimama toka kushoto, John Kitime(guitaa na kuimba),sasa yuko Kilimanjaro Band-Wananjenje, Dereva wa msafala,Marehemu Aggrey Ndumbalo (Rhythm gitaa, Mhasibu), Abuu Semhando (Drummer) s Twanga Pepeta, Maerehemu Freddy Benjamin (Muimbaji), Said Mnyupe (Trumpetist) sasa yuko msondo, Saidi Ndula (Saxophone, Rashid Pembe (saxophone), Hassan Shaw (keyboards).....Pambamoto awamu ya pili

Na Moshy Kiyungi, Tabora.
Septemba, 2019.

Mungu aliumba kusahau, lakini historia haiwezi kuashaulika katu. Inakaribia miaka 9, tangu maisha ya mwanamuziki Abuu Ally Semhando yalipokatizwa hata kabla ya kutimiza ndoto alizokuwa amejiwekea.

Ajali ya pikipiki aliyokuwa akiiendesha mwenyewe, aliyopata nayo ajali akitokea kazini, iliyopelekea kifo chake Desemba 18, 2010, jijini Dar es Salaam akiwa ametimiza umri wa miaka 57.
Semhando wakati wa uhai wake alichangia mafanikio ya Kampuni ya African Star Entertainment Tanzania (ASET), kwa asilimia kubwa kutokana na kujitoa kwa kila hali.
Alidumu kwa kipindi kirefu katika bendi hiyo toka alipojiunga mwaka 1998, akitokea katika bendi ya Diamond Sound ‘Wana Kibinda Nkoi’.

Kifo chake kiliwatia simanzi watu wengi hususan mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya ASET Asha Baraka, aliyemuelezea Abuu kuwa aliitumikia Twanga kwa mapenzi makubwa kama mali yake binafsi.
Asha alitamka kuwa Semhando alikuwa ni chachu ya mafanikio ya albamu zote 10, ambazo wamezitoa kutokana na kushiriki katika kuandaa muziki na kusimamia nidhamu ya wanamuziki wa bendi hiyo.
Kifo cha Abuu Semhando katika familiya yake, kiliigusa kwa kiasi kikubwa hususan binti yake Sharifa, ambaye siku ambayo alikuwa anatakiwa kufungishwa ndoa, ndiyo siku baba yake mauti yalipomfika, sherehe hizo zikageuka msiba mkubwa.
Wasifu wa nguli huyo unaeleza kuwa jina lake kamili lilikuwa akiitwa Abuu Ally Semhando maarufu ‘Lokassa’ au ‘Baba Diana’
Alikuwa mcharazaji mahiri wa drums wakati huo huo alikuwa ndiye meneja wa bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’.
Abuu Ally Semhando ‘Lokassa’ alizaliwa mwaka 1953 Kijiji cha Kibanda Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.
Alianza shughuli za muziki mwanzoni mwa miaka 1970, akiwa katika bendi ya Tanga International iliyokuwa ikitoa burudani mjini humo wakati huo.
Baadaye alikwenda kuwa mmoja kati ya waasisi wa bendi za Tanza Muzika na Orchestra Tomatoma kabla ya kutua Safari Sound Orchestra (OSS).
Abuu Semhando na Hamza Kalala ni miongoni mwa wanamuziki waanzilishi wa bendi ya Super Matimila, ni hao waliowakaribisha marehemu Mose Sengo Fan Fan na Dk. Remmy Ongala katika bendi hiyo.
Katika pilika za kutafuta maisha, Semhando alikwenda kujiunga na bendi ya Vijana Jazz ‘Pamba Moto’, ambako huko alionekana kuwa anao uwezo mkubwa wa kuongoza, akakabidhiwa nafasi ya kuwa Katibu wa bendi.
Semhando alishiriki kupiga drums kwa kiwango kikubwa katika nyimbo nyingi ambazo ziliiletea mafaniko bendi hiyo ya Vijana Jazz.
Aliyekuwa mtunzi na mwimbaji maarufu toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Selemani Kasalo Kyanga, alimpachika jina bandia la ‘Lokassa’, wakiwa katika bendi ya Tancut Alimasi iliyokuwa na makazi yake mjini Iringa.
Licha ya kuwa mpiga drums, Sembando alikuwa ni mwanamuziki mwenye kipaji kikubwa cha uongozi wa bendi.  
Alishiriki katika kuandaa muziki kila bendi aliyopitia alihakikisha inapata mafanikio makubwa. Jambo hilo lilimjengea umaarufu maradufu.
Historia inaonesha kuwa kila bendi alizowahi kupitia akiwa kiongozi baada ya kuondoka, ziliyumba na zingine kutokomea kabisa katika medani ya muziki wa dansi.
Lakini si Super Matimila pekee yake hata alipokuwa na Vijana Jazz ‘Saga rhumba’ ambako alikuwa Katibu chini ya uongozi wa Hemed Maneti, alikuwa mmoja wanamuziki walioshiriki katika kuiletea mafanikio kwa miaka yote hiyo kabla ya kujiondoa.
Yaelezwa kuwa Abuu pia akiwa na bendi ya Vijana aliasisi ‘Vijana Day’ iliyokuwa ikifanyika kwenye ukumbi wa Vijana Hostel, Kindondoni jijini Dar es Salaam.
Alishiriki kwa kiwango kikubwa kutengeneza mashairi ya nyimbo nyingi akiwa na waimbaji akina Hemed Maneti, Saidi Hamis ‘Misukosuko’, Fred Benjamin, Cosmas Chidumule na Kida Waziri.
Aidha Semhando alishirikiana vyema na wapiga ala wenzake wakati huo wakiwamo Kulwa wa Milonge, Hamza Kalala, Hassan Dalali, Agrey Ndumbalo, Rashid Pembe, Hassan Shaw na Disfa Semhando (mdogo wake), aliyekuwa akiliungurumisha gitaa la besi.
Aidha alikuwepo mpiga gita la solo Shabani Yohana “Wanted” na wengine wengi.
Akiwa na safu hiyo ambao ni baadhi tu ya kundi alilokuwa nalo, walishiriki kutengeneza nyimbo kali kama ‘Bujumbura’, ‘Mary Maria’, ‘Tambiko la Pambamoto’, ‘Mundinde’, ‘Ali Hassan Mwinyi apewe Kura za Ndiyo’, ‘Wifi Zangu Wananinyanyasa’, Stella, ‘Penzi haligawanyiki’ na nyingine nyingi nzuri kupindukia.
Nyimbo hizo zilitikisa medani ya muziki chini ya uongozi shupavu wa viongozi wake akina Hemed Maneti aliyekuwa kiongozi, Hamza Kalala alikuwa ni kiongozi msaidizi na Abuu Semhando mwenyewe  aliyekuwa Katibu.
Katika kudhihirikisha uwezo aliokuwa nao alipojing’atua katika bendi hiyo, ndipo jinamizi na anguko la bendi ya Vijana Jazz lilipoanza kuinyemelea.
Baadhi ya wanamuziki aliofanya nao kazi walimzungumzia marehemu Semhando akiwemo  John Kitime ambaye alisema kuwa ataendelea kumkumbuka Abuu Semhando kwa ucheshi wake.
Kitime aliwahi kutamka kuwa yeye alimpokea na kumtafutia malazi jijini mwaka 1989, wakati anajiunga na Vijana Jazz akitokea Tuncut Almasi ya Iringa.
Waliosimama..Remmy Ongala, Abuu Semhando, Kasaloo Kyanga, Fan Fan
Kwa upande wake mkung’utaji wa gitaa la solo Aldof Mbinga, hakusita kutamka kuwa tasnia ya muziki wa dansi imepoteza Jemedari ambaye alikuwa hayumbi katika misimamo yake jambo ambalo lilileta mafanikio kwa wanamuziki na bendi Vijana Jazz kwa ujumla.
Mbinga alifanya kazi na Semhando kwa kutengeneza albamu ya kwanza ya Twanga Pepeta ya ‘Kisa Mpemba’ na ‘Jirani’.
Wengine waliomzungumzia marehemu Semhanso ni pamoja na Waziri Ally ambaye ni mwanamuziki na kiongozi wa bendi The Kilimanjaro ‘Wana Njenje’, alimtaja Semhando kama nguzo iliyokatika ghafla wakati watu wakiihitaji huduma licha ya ukongwe wake katika muziki.
Ushuhuda mwingine ulitolewa Isihaka Kibene, ambaye alisema, Twanga Pepeta imepoteza mpiganaji na mtawala mahiri kutokana na kuwa kiungo katika kufanya majukumu ya kila siku ya bendi.
 “Huyu jamaa alikuwa rafiki yangu sana ambaye niliwahi kufanya naye kazi kiwanda cha Uchapaji cha Printpak miaka ya 1970, na hata alipoanza shughuli za muziki tuliendelea kuwa marafiki..." alisema Kibene.
Abuu Ally Semhando aliacha mjane na watoto 10, alizikwa kijijini Kibanda Wilaya ya Muheza moani Tanga alikozaliwa.
Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0736331200, 0713331200 na 0767331200


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/302iEKQ
via

Post a Comment

0 Comments