Bashe, Ndugai walivalia njuga Korosho, waapa kulikuza zao hilo kuwa la kibiashara

  Masama Blog      
Charles James, Michuzi TV

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Hussein Bashe ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kuanzisha kituo maalumu cha kukuza kilimo cha korosho ikiwa ni baada ya kuzindua mkakati mahususi wa kulifanya zao hilo kuwa la kimkakati.

Mhe Bashe ameyasema hayo wakati alipohudhuria Baraza la Biashara na Wadau wa Kilimo katika kuhamasisha kilimo cha korosho na mtama Wilaya ya Kongwa.

Katika mkutano huo Mhe Naibu Waziri alimtaka Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho hadi kufikia Oktoba 15 awe amehamisha kituo cha pembejeo za korosho kilichopo Wilaya ya Mpwapwa kinahamia Wilaya ya Kongwa na haswa eneo la Kibaigwa kwa sababu ndipo mahitaji ya zao hilo yapo kwa asilimia kubwa.

Mhe Bashe alimuahidi Spika wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, Job Ndugai kuhakikisha analisimamia zoezi hilo na kwamba yeye mwenyewe atafika wilayani hapo Oktoba 15 kushuhudia kituo hiko kikianzishwa.

" Naiagiza Halmashauri kupitia Mkurugenzi kuanzisha vituo vidogo vijijini ambavyo vitakua na kazi ya kuzalisha mbegu za korosho ili kuwarahisishia wakulima badala ya kufuata mbegu hapa Kibaigwa wawe wanazipata ndani kwenye maeneo yao.

" Ndugu zangu wakulima, mimi niwahakikishie sisi kama Wizara tumejipanga haswa. Suala la upatikanaji wa mbegu, madawa na elimu ya zao hili tunaitoa kwa kasi na kwa namna ambayo kila Mwananchi atanufaika. Tumuunge mkono Rais wetu kwa kulipigania zao hili la Korosho," amesema Naibu Waziri Bashe.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo, Mh Job Ndugai amewataka viongozi wa Dini, Chama na Serikali kulivalia njuga zao la kilimo kwani kupitia utafiti uliofanyika unaonesha Wilaya ya Kongwa ina Ardhi nzuri ya kufanya kilimo hicho ambacho yeye anaamini ndio Dhahabu ya Kongwa.

Amesema kama viongozi wana wajibu mkubwa wa kuwa mfano kwa wananchi katika kulipambania zao hilo kwa kupanda mikorosho ambapo amewaonya pia viongozi ambao wana mpango wa kugombea mwakani kuwa watapitishwa na chama kwa kuangalia ushiriki wao katika kulikuza zao hilo.

" Mimi ni mjumbe wa kamati kuu, mwakani kama haujalima korosho basi ujue jina lako tutalikata. Sisi kama viongozi tuna jukumu zito la kukuza zao hili la korosho na kulifanya kuwa zao la Biashara.

" Simaanishi tuache kufanya kilimo kingine lakini ndugu zangu nawaambia kwa Dunia ya sasa biashara ya kilimo hivi sasa ipo kwenye mazao ya miti. Ndio maana unaona maeneo yenye maparachichi, mapapai, kahawa wanafanikiwa zaidi. Tuamke sasa na kuikijanisha Kongwa yetu kwa kupanda Mikorosho," amesema Mhe Ndugai.
 Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika wa Bunge, Mhe Job Ndugai akizungumza kwenye Baraza la Biashara na Wadau wa Kilimo cha Korosho na Mtama ambapo amewataka viongozi wa Kisiasa, Kidini na Serikali kushirikiana kukuza zao hilo
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe akizungumza wakati wa Baraza la Biashara na wadau wa kilimo cha korosho na mtama wilayani Kongwa.
 Wananchi, wakulima na watumishi wa Serikali waliojitokeza kwenye mkutano huo was Baraza la Biashara la Wilaya ya Kongwa.
 Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi akizungumza katika mkutano maalumu wa Baraza la Biashara la Wilaya hiyo
 Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe Deo Ndejembi akihutubia wananchi, wakulima na watumishi waliojitokeza kwenye mkutano maalumu wa Baraza la Biashara la Wilaya hiyo.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2LyWPNA
via
logoblog

Thanks for reading Bashe, Ndugai walivalia njuga Korosho, waapa kulikuza zao hilo kuwa la kibiashara

Previous
« Prev Post