Ticker

10/recent/ticker-posts

RAIS DK MAGUFULI AKABIDHIWA UENYEKITI SADC , HOTUBA YAKE GUMZO KWA WAKUU WA NCHI WANACHAMA

*Asema Bara la Afrika lina kila aina ya rasilimali , sio masikini 
*Aiambia Jumuiya ya Kimataifa iondoe vikwazo kwa Zimbabwe 

Na Said Mwishehe, Michuzi TV 

MWENYEKITI mpya wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC) Rais Dk.John Magufuli ameziambia nchi za jumuiya hiyo kuwa Bara la Afrika si masikini kwani lina utajiri wa kila aina unatokana na silimali zake. 

Pia ametumia nafasi hiyo kuitaka Jumuiya ya kimataifa kuondolea vikwazo nchi ya Zimbabwe ambayo imewekewa kwa muda mrefu na athari ambazo zinaipata nchi hiyo inaathiri na nyingi nyingine za Afrika. 

Akitoa hotuba yake ya kwanza baada ya kukabidhiwa Uenyekiti wa SADC leo katika Mkutano Mkuu wa 39 wa jumuiya uliofanyika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Rais Magufuli ametoa muelekeo mpya kwa jumuiya huyo kwa kueleza mambo mbalimbali. 

BARA LA AFRIKA SIO MASIKINI 

Mwenyekiti huyo mpya wa SADC amewaambia wakuu wan chi hizo pamoja na viongozi wa Serikali kwamba Afrika sio masikini kwani ina kila kitu zikiwemo rasimali za kutosha ambazo zinatoha kufanya maendeleo. 

“Inasikitisha kuona nchi za Afrika zikiwemo za SADC zinaendelea kujiita maskini wakati zimejaaliwa rasilimali watu, ardhi, maji, madini na misitu. Rasilimali zilizopo zikitumika vizuri Bara hili haliwezi kuendelea kuwa maskini na ombaomba kwani zinahitajika duniani kote. 

Amesema nchi za Bara la Afrika ikiwemo jumuiya ya SADC inayo nafasi ya kuhakikisha kupitia raslimali zilizopo maendeleo yanapatikan.”Afrika sio masikini kwani tunakila kitu.” 

“Nimepokea kijiti cha Uenyekiti kutoka kwa Rais wa Namibia Dk. Hage Geingob na nijipanga kusimamia eneo la viwanda ili kuleta tija kwa maendeleo ya Kanda hiyo. Mwenyekiti aliyemaliza muda wake ameweka mazingira mazuri katika sekta ya miundombinu na vijana, hivyo ni lazima kuwepo na jitihada za kila nchi kujikita katika ujenzi wa viwanda kwa kasi kubwa. 

Amefafanua madhumuni ya waasisi wa SADC yalikuwa yamejikita kupigania amani, ulinzi na siasa na sasa ni jukumu la jumuiya hiyo kuleta maendeleo kwa ajili ya wananchi wake. 

“Nikiwa kama Mwenyekiti mpya nitahakikisha suala la amani na ulinzi linakuwepo lakini ni nipende kueleza tunapaswa kujikita katika viwanda ili kufikia malengo ya kijamii na uchumi kwa haraka,” amesema Dk.Magufuli. 

Amesema mwaka 2018 SADC ilikuwa imejipangia kuwa na uchumi wa zaidi ya asilimia 7 lakini imefikia asilimia 3.1 hiyo ikiwa ni chini ya asilimia ya Umoja wa Afrika (AU) iliyofikia asilimia 3.5 na Afrika Mashariki asilimia 5.7, Afrika Kaskazini asilimia 4.9 na Afrika Magharibi asilimia 3.3. 

“Biashara ya nje ya kanda mwaka 2017 nchi za SADC zenye watu zaidi ya milioni 370 na ukubwa wa heka zaidi ya milioni 9.8 ilisafirisha bidhaa nje ya nchi zake za dola za Marekani bilioni 143 huku ikiwa na rasilimali zote jambo ambalo sio zuri. 

“Haingii akilini kuona nchi mbili Mexico na Vietnam ambazo watu wake hawazidi milioni 132 na eneo lisilozidi ukubwa wa hekta 1.9 ukubwa wa zaidi ya lakini imesafirisha bidhaa zenye thamani zaidi ya dola za Marekani bilioni 403 hali ambayo inaashirikia kuwa SADC haifanyi vizuri,”amesema. 

Hata hivyo amesema kiuhalisia nchi wanachama zinapaswa kujipanga na kufikia malengo yake ikiwa ni kuhakikisha zinajenga viwanda ili kuandaa bidhaa zinazotokana na mazao zinakuwa na viwango vinavyokubalika na kuachana na kuuuza malighafi. 

“Hakuna sababu ya kuficha kwani ndio hali halisi kuwa katika eneo hilo hatujafanya vizuri tunapaswa kujipanga ili kushindana na soko la dunia,”amesema Rais Magufuli. 

Pia amesema jambo la kusikitisha ni kuona nchi wanachama wa SADC zimekuwa zikiagiza bidhaa nyingine kutoka nje ya nchi wanachama hali ambayo inakwamisha mipango ya kuendelea na kukuza uchumi baina yao. 

Ameongeza uchunguzi wake amebaini kitendo cha nchi za SADC kuagiza vyakula kutoka nje ni kutokana na kukosekana kwa taarifa, hivyo kuna mahali ambapo hawapo sawa katika kutoa taarifa. 

Amesema nchi za SADC zinazalisha mazao mengi lakini kinachoonekana ni kuendelea kuewa na mtazamo wa kufikiria kuwa bila kuagiza nje huwezi kupata bidhaa bora. 

“Nilifanya ziara hivi karibuni katika nchi tatu za SADC ambazo amezikuta na ukame na majanga .Nimekuta zikiagiza chakula kutoka nje huku Tanzania, Afrika Kusini, Angola na Mauritius na nyingine zikiwa na akiba ya chakula zaidi ya tani milioni mbili hii si sawa tunapaswa kubadilika,” amesema. 

Ameongeza changamoto nyingine ambayo ameibani kukwamisha maendeleo na kukuwa kwa uchumi kwa nchi wanachama ni kutokana na kuwepo kwa sheria, sera na kanuni ambazo haziwiani hivyo kukwamisha biashara. 

“Ni lazima kuwepo na uhuiwishaji wa sheria na sera za nchi wanachama ili isiwe sababu ya kukwamisha maendeleo yao wenyewe kama ilivyo sasa.Pamoja na hizo changamoto ambazo nimezianisha ipo nyingine ya kukosekana kwa viwanda. 

“Hakuna nchi ambayo imeendelea duniani bila kuwepo viwanda, kwani takwimu zinaonesha nchi zenye viwanda zinauza bidhaa nyingi zaidi ya nchi ambazo hazina viwanda,” amesema. 

Amesema nchi za SADC zinauza malighafi zaidi hali ambayo inakwamisha mipango na mikakati hivyo ni jukumu la kila nchi kuhakikisha kuwa zinakuwa na viwanda vitakavyopandisha thamani ya mazao yao. 

“Suala la viwanda litakuwa kipaumbele changu cha kwanza katika uenyekiti wangu, hivyo naomba ushirikiano, lakini yote hayo yanaweza kufanikiwa iwapo tutadhibiti rushwa na kusimamia makubaliano tunayokubaliana, kwani nchi zetu sio masikini,” amesema. 


AITOLEA UVIVU SEKRETARIETI YA SADC 

Wakati huo huo Rais Magufuli ameitaka jumuiya hiyo kuhakikisha inasimamia vema majukumu yake kwani haridhishwi na utendaji wake na kuitaka ijitathmini upya. 

Amefafanua sekretarieti hiyo imeshindwa kuja na mipango ambayo inaweza kusaidia nchi wanachama kukuwa kiuchumi na maendeleo kama ambavyo inapaswa kufanya. 

Amesema changamoto zote ambazo amezitaja zinapaswa kushughulikiwa na sekretarieti kwa kuja na majibu ikiwa ni pamoja kwanini GDP inashuka kila siku katika kipindi ncha miaka 10 sasa huku miaka ya nyuma ilikuwa inapanda mwaka hadi mwaka. 

“Kuanzia mwaka 2009 uchumi umekuwa ukikua kwa kiwango kisichozidi asilimia 5 tofauti na mwaka 2005 hadi na 2009 ambapo ulifika hadi asilimia 7, hivyo sekretarieti kuitaka ijitafakari na kuja na majibu sahihi wapi imekosea,”amesema. 

ATAKA ZAMBABWE IONDOLEWE VIKWAZO 

Mwenyekiti wa SADC ameziaomba jumuiya za kimataifa kuondoa vikwazo ilivyoweka kwa nchi ya Zimbabwe kwa kuwa vikwazo hivyo vinaumiza nchi za SADC. Amesema vikwazo vya Zimbabwe ni vikwazo ambavyo athari zake zinakwenda kwa Afrika yote, hivyo lazima wawe na kauli moja ili jumuiya ya kimataifa kuondolea vikwazo. 

MWENYEKITI ALITEMALIZA MUDA WAKE 

Kwa upande wake Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Rais wa Namibia Dk. Hage Geingob, amesema anashukuru ushirikiano aliopewa na viongozi wenzake na kufaikisha kusimamia amani kwa kipindi chote. 

Amesema mwaka mmoja ya uogozi wake ameshuhudia chaguzi sita katika nchi za Malawi, DRC Congo, Madagascar, Afrika Kusini, Comoro na Eswatini ambazo zimefanyika kwa uhuru na haki. 

Dk. Geingob amesema nchi za SADC zimefanikiwa kusaidia majanga ya asili yaliyotokea nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Madagascar na wamekuwa wakijifunza kila siku namna ya kukabiuliana na hali hiyo. 

“Mwaka mmoja wa uongozi wangu nimefanikiwa kuja na proramu ya kuwezesha vijana katika ushiriki kwenye mijadala na maamuzi ambayo yanagusa jumuiya hiyo. 

“Tumeweza kusimamia utekelezaji wa mkakati wa uwepo wa miundombinu ya viwanda ikiwa ni mkakati wa 2015 hadi 2063.Naamini Mwenyekiti mpya ataendeleza ili siku moja SADC iwe kanda ya viwanda vya kisasa,”amesema.
Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Rais Dk.John Magufuli  akitoa hotuba yake ya kwanza baada ya kukabidhiwa Uenyekiti wa SADC leo katika Mkutano Mkuu wa 39 wa jumuiya  hiyo uliofanyika katika kituo cha Kimataifa cha mikutano cha Julius Nyerere,jijini Dar.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), aliyemaliza muda wake Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob, akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt John Pombe Magufuli baada ya kumkabidhi 'kijiti' cha Uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwenye mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi leo Jumamosi Agosti 17, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo, Dk Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), aliyemaliza muda wake Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob, akimvisha wadhifa huo Rais Dk John Magufuli kwenye mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi leo Jumamosi Agosti 17, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu Mtendaji wa jumuiya hiyo, Dk Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi.



from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2Zfe6jS
via

Post a Comment

0 Comments