Ticker

10/recent/ticker-posts

MWENYEKITI ALIYEMALIZA MUDA WAKE SADC DK.GEINGOB AHIMIZA NCHI WANACHAMA KUWASHIRIKISHA VIJANA KULETA MAENDELEO

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MWENYEKITI ambaye amemaliza muda wake wa kuiongoza Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC) Rais wa Namibia Dk.Hage Geingob amezitaka nchi wanachama kuhakikisha vijana wanapewa kipaumbele katika nyanja mbalimbali kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Amesema robo tatu ya wananchi wa jumuiya hiyo wana umri chini ya miaka 27 na hivyo kundi hilo la vijana likipewa nafasi kwenye zao kuna uwezekano mkubwa kwa nchi hizo kupiga hatua.

Dk.Geingob ameyasema hayo leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kabla ya kukabidhi uenyekiti wa SADC kwa Rais wa Serikali ya Tanzania Dk.John Magufuli.

Ambapo wakati anazungumzia mikakati mbalimbali ya jumuhiyo ili ipige hatua kimaendeleo ameeleza umuhimu wa vijana kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika msafara wa maendeleo

Amesisitiza robo tatu ya wananchi wa jumuiya hiyo ni vijana, hivyo wakitumika vizuri itasaidia kuleta maendeleo.

"Ni muhimu nchi zetu zikaweka mkazo na kutia maanani vijana kupata nafasi.Wanao uwezo mkubwa ulioambatana na ubunifu.Hivyo lazima tuwatumie kikamilifu kwa maendeleo yetu.

", Ukweli ni kwamba lazima twende pamoja na vijana wetu, tushirikiane kwa kila hatua.Naamini vijana wakitumika kikamilifu nchi zetu zitapiga hatua kubwa kimaendeleo.Tunayo changamoto ya ajira kwenye nchi zetu,vijana wamekuwa wakikimbilia nchi za Ulaya,umefika wakati wa kuwashirikisha vijana kutatua changamoto zetu," amesema.

Mbali ya kuzungumzia umuhimu wa vijana kutumika kuleta maendeleo,Mwenyekiti huyo aliyemaliza muda wake ameeleza haja ya nchi hizo kuweka mikakati ya kuboresha miundombinu na huduma za jamii kwa ajili ya wananchi huku akihimiza uongezaji thamani kwa mazao yanayozalishwa kwa nchi wanachama.

Pia amesema kuna haja ya kuwepo na mfumo thabiti wa kiabiashara baina ya nchi hizo na kwamba kwa kufanya hivyo uchumi utaimarika na kupiga hatua.

Wakati huo huo amesema kuna kila sababu ya kuongeza jitihada za kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafanikiwa.Ametumia nafasi hiyo kueleza Serikali za jumuiya hiyo kuwa na sera ambazo zinakuza uchumi wa wananchi na kwamba sekta binafsi zipewe nafasi ya kushiriki kuleta maendeleo.

"Sekta binafsi ipewe nafasi yake.Tukizipa nafasi sekta binafsi tutapiga hatua ya maendeleo kwa nchi zetu," amesema Dk.Geingob na kuongeza jambo la kufurahisha nchi hizo zimeendelea kushirikiana hatua kwa hatua.

Akizungumza zaidi kuhusu jumuiya hiyo Dk.Geingob amesema kwamba nchi za SADC zinatambua na kuthamini mchango wa Baba wa Taifa la Tanzania Hayati Julius Nyerere kwa namna ambavyo alijitoa kufanikisha nchi nyingi za Afrika zinakuwa huru.

Pia amezungumzia ukuaji wa demokrasia kwa nchi za jumuiya na kufafanua ndio maana nchi nyingi marais wake wamepatikana kutokana na chaguzi huru na leo wameshiriki mkutano wa 39 wa SADC.

Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa historia ya ncho hizo inafanana na kubwa zaidi amani na mshikamano vimeendelea kuimarika.Wakati huo huo amesema pamoja na hatua mbalimbali za kuleta maendeleo,nchi nyingi za jumuiya hiyo zimeendelea kukumbwa na maafa na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo amezishukuru nchi za jumuiya hiyo namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana na kusaidiana kukabiliana na majanga yanayotokea na hasa vimbunga na mafuriko.

Amezitaka nchi za SADC kuhamasisha wananchi kutunza mazingira kwa kutokata miti hovyo na kuwahamasisha kuoanda miti kwa wingi kama njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
 Mwenyekiti amaye amemaliza muda wake wa kuiongoza Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC) Rais wa Namibia Dk.Hage Geingob akihutubia kwenye mkutano huo leo uliofanyika Katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere,jijini Dar,Dkt Hage amekabidhi Kijiti kwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.Picha na Michuzi JR.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/31MqQjg
via

Post a Comment

0 Comments