Ticker

10/recent/ticker-posts

AGIZO LA RAIS MAGUFULI LAZAA MATUNDA HANDENI.,SOMA ZAIDI HAPA

Ni baada ya kukamilika kwa bwawa lililopo mkata na kuhudumia wananchi wa maeneo hayo ambapo bwawa hilo miongoni mwa mabwawa 3 ambayo yalitolewa maagizo ya kusimamiwa na kukamilika na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh John Pombe Magufuli wakati alipokuwa kwenye ziara zake wilayani Handeni mwaka 2017.

Kufuatia Agizo hilo la Rais Magufuli, Serikali ya wilaya ya Handeni imesimamia vyema ambapo hadi kufikia sasa bwawa la mkata limekamilika kwa 100% na hivyo kuanza kuhudumia wananchi wa eneo hilo huku bwawa la Kwagunda likifikia 75% ambapo mkandarasi ameagizwa kukarabati tuta ambalo ni kuzuizi cha kupotea kwa maji ya bwawa hilo ili kufikia 100% ya ukamilishaji ambapo kwa upande wa bwawa la Manga wananchi wameomba fedha zake zitumike kutoa maji kutoka kwenye chanzo cha Mto Ruvu/Wami kilichopo chalinze na kuyasafirisha hadi kufika mkata ambapo hiyo itasaidia wananchi kupata huduma ya maji ya uhakika kwa vipindi vyote.

Mkuu wa wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe ametembelea  vituo hivyo 15 vinavyotoa maji katika eneo hilo la mkata ikiwa ni muendelezo wa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo na kukuta wakinamama wengi wakichota maji.Mkuu wa Wilaya ameielekeza Halmadhauri ya wilaya ya Handeni kuhakikisha inaongeza idadi ya vituo vya utoaji wa maji. "Ili kuondoa msongamano kwa kila kituo cha kuchotea maji ni lazima Halmashauri ya Wilaya Handeni iongeze idadi ya vituo vya maji vingine 33 ili kufikia vituo vya maji 48 kama ramani ya mtandao wa maji ya mwanzo ilivyoelekeza na hili litekelezwe mapema", Alisisitiza Mh.Gondwe.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Handeni ndugu William Makufwe amethibitisha kuanza mapema iwezekanavyo utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Wilaya la kuongeza vituo vya kuchotea maji wananchi Mkata."Fedha ipo na utekelezaji utaanza mapema ili huduma ya maji iwafikie wananchi wa Mkata na ukosefu wa maji uwe historia katika eneo hili", alisema.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliokuwa wakipata huduma maji wameishukuru sana Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais wake John Pombe Magufuli kwa utekelezaji wa ahadi mbalimbali ikiwemo maji ambapo kwa sasa wananchi wanapata huduma bora ya maji tofauti na kipindi cha nyuma.

 _"Zaidi ya miaka 15 iliyopita maji yamekuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi wa wilaya ya Handeni lakini sasa Uongozi wa Serikali ya wilaya umefanikiwa kupambana na changamoto hiyo na hatimae changamoto hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa"._