Ticker

10/recent/ticker-posts

Serikali Yakana Kuitenga Mikoa ya Kanda ya Kaskazini

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Tano haijaitenga mikoa ya Kanda ya Kaskazini kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidai.

Samia amesema kumekuwapo na dhana potofu iliyojengwa na baadhi ya watu kuwa Mkoa wa Kilimanjaro umetengwa, jambo ambalo halina ukweli.

Amesema Serikali haijawatenga wananchi na ndiyo maana miundombinu kama ya barabara na afya imekuwa ikitekelezwa.

Makamu huyo wa Rais aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Pasua, Manispaa ya Moshi alipoweka jiwe la msingi la upanuzi wa jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya Pasua akiwa katika ziara mkoani humo.

Alisema Serikali haiwezi kuwatenga wananchi wa mikoa hiyo kutokana na itikadi za kisiasa, bali jukumu lake ni kuwahudumia Watanzania wote katika kuhakikisha wanapata huduma bora za kijamii.

“Ondoeni dhana kuwa mikoa ya Kaskazini imetengwa, hii siyo kweli, Serikali haiwezi kuwatenga, Kaskazini ipo Tanzania, uchaguzi uliopita mmeleta wabunge wachache wa Chama cha Mapinduzi ndio maana wako wachache,” alisema.

Alisema, “Serikali yetu ni ya uwazi na ukweli, nafasi za mawaziri Kilimanjaro mmetuletea? Lakini mngetuletea wengi, mawaziri wangekuwa wengi, mmetuletea wachache ndio maana wako wachache.”

Makamu wa Rais alisema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo nchi nzima ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.

“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wananchi wanapata maisha bora kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ilikuwa ni kero kubwa kwa wananchi ikiwemo miradi ya umeme, miundombinu ya barabara, afya, elimu na maji,” alisema.

Awali, aliwataka wananchi kutunza miundombinu ya barabara inayojengwa na Serikali kwa sababu inatumia gharama kubwa.

Samia aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Barabara ya Bonite mjini Moshi iliyojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa zaidi ya kilomita 2.9 ambayo imegharimu zaidi ya Sh 3bilioni.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri na bora.