Ticker

10/recent/ticker-posts

Benki ya Dunia Yaipatia Tanzania Bilioni 680 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu

Benki ya Dunia imeridhia kuipatia Tanzania Dola za Marekani milioni 300 (Sh. bilioni 680.5) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya sekondari.

Fedha hizo zinakusudiwa kutumika kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maabara, nyumba za watumishi na kununua vifaa vya kufundishia.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Dk. Hafez Ghanem, alisema hayo jana alipokutana na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Dk. Ghanen alisema pamoja na kuridhia kutoa fedha hizo, benki hiyo inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.2 (zaidi ya Sh. trilioni 13) na kwamba miradi hiyo inatekelezwa kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri kati yake na Tanzania.

Dk. Ghanem alisema katika mazungumzo hayo, walijadili juu ya maendeleo ya miradi hiyo na kazi nzuri ambayo inafanywa na Tanzania kuimarisha uchumi. Pia alimpongeza Rais Magufuli kwa matokeo mazuri katika mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha huduma za jamii.

Kwa upande wake, taarifa hiyo ilisema, Rais Magufuli aliishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano na uhusiano mzuri na Tanzania na kuahidi kuwa serikali itaendeleza na kukuza uhusiano huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo zinatumika kwenye miradi iliyokusudiwa.

“Namshukuru Dk. Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania. Hizo Dola Milioni 300 ambazo baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali, anasema zitaletwa.

“Pia Benki ya Dunia imetoa Dola bilioni 5.2 ambazo zinafadhili miradi mbalimbali ya elimu, nishati, barabara, kilimo, afya na maji, ni miradi mikubwa na mingi. Kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha,” alisema Rais Magufuli.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, aliitaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kuwa ni pamoja na uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 24.

Aliitaja mingine kuwa ni ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara eneo la Ubungo, jijini Dar es Salaam na ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kwa awamu ya kwanza na ya pili.

Mazungumzo kati ya Mhe. Rais Magufuli na Dk. Ghanem yalihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga; Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi; Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako; Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu; na Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Bella Bird.