Ticker

10/recent/ticker-posts

Shirika La Ndege Tanzania (ATCL) Limeondolewa Vikwazo hivi muhimu sana Duniani ..Soma Hapa

 Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeruhusiwa kurejea katika Shirikisho la Mashirika ya Ndege Duniani (IATA), ambapo kuanzia sasa litakuwa na uwezo wa kuuza tiketi zake duniani kote.

ATCL iliondolewa IATA miaka tisa iliyopita baada ya kuelemewa na mzigo wa madeni.

Lakini tangu kufufuliwa upya kwa shirika hilo 2016, limekuwa likipambana kutaka kurejea upya katika uanachama ili kuepuka kukosa malipo ya tiketi zao hususan katika safari za kimataifa.

Taarifa ya ATCL iliyotolewa kwa washirika wake Oktoba 24 na kuthibitishwa na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Ladislaus Matindi jana  inaeleza kuwa, kurejeshwa kwao kumeanza rasmi mwezi huu.

“Tulipata taarifa kutoka IATA kuwa tumerudishwa kwenye mfumo wa malipo wa pamoja (Airlines Clearing House - ACH)), na sasa Air Tanzania imerejea katika mfumo huo na ni mwanachama halali wa shirikisho hilo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na mkurugenzi wa Fedha, Albinus Manambu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa fomu zote za malipo ambayo hayakufanyiwa kazi au kulipwa wakati ATCL ilipoondolewa katika mfumo, zinapaswa kutumwa upya ACH ili ziweze kushughulikiwa.

Akizungumzia kurejea IATA, mkurugenzi wa Biashara wa ATCL, Patrick Ndekana alisema hatua hiyo inarahishisha uhusiano wao na mashirika pamoja na kampuni zingine za ndege katika biashara kwa kuwa wanapenda kushirikiana na watu waliopo IATA.

“Soko letu katika huduma litapanuka zaidi na tutaweza kushindana na kuifanya Dar es Salaam kuwa njia pana ya kuelekea maeneo mbalimbali, sasa tutafahamika kimataifa na tutaweza kuingia makubaliano na mashirika makubwa ya ndege,” alisema Ndekana.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ni muhimu kibiashara hususan wakati huu ambao wamelenga kupanua safari zao nje ya mipaka ya Tanzania.

Alisema kutokana na kurejeshwa IATA, hivi sasa abiria anaweza kukata tiketi za ATCL kokote duniani.