WAZIRI WA AJIRA JENISTA MHAGAMA AMFUKUZA KAZI MKANDARASI DAR......ATOA MASAA 6 KWA MKURUGENZI WA KINONDONI

  Eliafie Elifura      

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amemtimua kazi mkandarasi anayejenga mfereji wa Buguruni kwa Mnyamani, Manispaa ya Ilala kwa kushindwa kuujenga kwa kiwango kinachotakiwa.

Mbali ya kuchukua hatua hiyo jana, pia Waziri Mhagama aliagiza mkandarasi huyo asilipwe chochote.

Akiwa Tegeta, waziri huyo alimbana Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Ando Mwankuga na kumpa saa sita ampelekee taarifa ya ujenzi wa mfereji wa Tegeta – Basihaya uliojengwa chini ya kiwango.

Maeneo hayo ni yale ambayo miezi saba iliyopita, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliagiza ijengwe mifereji haraka ili kunusuru uhai wa wananchi waliokuwa wanasumbuliwa na mafuriko ya mara kwa mara.

Machi 24, Kikwete aliagiza kuvunjwa kwa nyumba zilizojengwa juu ya karavati lililoziba na kusababisha maji kujaa kwenye nyumba za wakazi wa maeneo hayo, agizo ambalo bado halijatekelezwa.

Mvua iliyonyesha siku mbili zilizopita ilisababisha nyumba 200 za eneo la Basihaya - Tegeta kukumbwa na mafuriko na nyingine 500 za eneo la Buguruni kwa Mnyamani zikiwa hatarini.

Mafuriko ya wakati huo yalitokana na mvua zilizonyesha kwa wiki mbili mfululizo na kusababisha vifo vya watu 12 huku mamia wakikosa makazi yao. Kutokana na hali hiyo, Mhagama aliagiza wahandisi waliosimamia mradi wa Basihaya, kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kisheria akiwaita ni ‘wahandisi mizigo’.

Akiwa Buguruni kwa Mnyamani, Mhagama alishuhudia ujenzi wa mfereji wa maji ulio chini ya kiwango huku ukiwa haujakamilika. Mfereji huo uliokuwa ukitakiwa kukamilishwa kwa miezi mitatu tangu Mei, ungegharimu Sh300 milioni.

“Huu ni utani wa maisha ya Watanzania. Imepita miezi mingi hapa katikati na jua lilikuwa linawaka. Ina maana mkurugenzi na mkandarasi hamjawahi kuja kuona nini kinaendelea? Naagiza huyu mtu asiendelee kujenga na wala asilipwe hata shilingi mia moja. Kama mlishamlipa, fedha hizo mtaifidia Serikali,” alisema Mhagama.

Aliwatahadharisha kuwa ikiwa mvua zitanyesha na kusababisha maafa kwenye eneo hilo kabla mfereji kukamilika, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Isaya Mungulumi na Mhandisi wake, Jaffari Bwigane watawajibika.

Ikiwa mfereji huo utajengwa kwa uhakika, utasaidia kunusuru watu zaidi ya 1,163 wa eneo hilo, kukumbwa na mafuriko kama kipindi kilichopita.

Katika ufafanuzi wake, Mungulumi alisema walibaini kuwa mkandarasi huyo ameshindwa kujenga kwa kiwango wiki mbili zilizopita na kwamba, tayari walianza kumchukulia hatua.

Aliilalamikia Sheria ya Ununuzi ya Umma kuwa ndiyo iliyowafanya kumpa muda wa wiki mbili ajirekebishe kabla ya kumtimua kama ilivyofanyika. “Bado hatujamlipa kiasi chochote cha fedha kwa sababu mkataba wetu ni ujenzi kwanza, ndipo alipwe,” alisema.

Akiwa Tegeta Basihaya, Mhagama alisema: “Wahandisi mizigo wanaoshindwa kusimamia miradi muhimu kama hii lazima wachukuliwe hatua za kisheria. Wote wavunjaji wa sheria na wanaoshindwa kusimamia sheria hawawezi kuendelea kuwa chanzo cha maafa kwa watu wengine.”

Alimtaka Mkuu wa wilaya hiyo, Paul Makonda kusimamia suala hilo ili kunusuru maisha ya wananchi kwani nyumba 200 zimezingirwa na maji.

Alisema haiwezekani mvua ya saa chache ikasababisha mafuriko kwenye eneo ambalo tayari Kikwete alishatoa maelekezo.

Kikwete aliagiza Manispaa ya Kinondoni kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye mkondo wa maji katika eneo hilo, agizo ambalo halikutekelezwa. Kutokana na hali hiyo, Mhagama aliagiza zibomolewe.

Makonda alikiri ujenzi huo kutokuwa wa kiwango: “Nashukuru waziri umekuja, ni kweli wapo watendaji mizigo kwenye halmahauri yetu, hasa hawa wasimamizi wa miradi kama hii inayojengwa kuokoa maisha ya wananchi.”

Katika taarifa aliyoitoa kwa Kikwete, Makonda alisema mradi huo ili ukamilike ungehitaji zaidi ya Sh3 bilioni. Jana Diwani wa kata ya Kunduchi, Michael Urio alisema kuwa Sh1.2 bilioni zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambao bado unahatarisha maisha ya wananchi wa eneo hilo.

Kaimu Mkurugenzi, Mwankunga alisema upungufu uliojitokeza kwenye mradi huo utarekebishwa. “Kabla ya saa kumi (jana) tutampelekea Waziri taarifa ya ujenzi wa mradi huu kama alivyotuagiza. Kuhusu makandarasi mizigo tutachunguza ikiwa wapo basi hatua za kinidhamu zitachukuliwa,” alisema.

Injinia wa umwagiliaji wa Manispaa hiyo, Fransis Mugisha alisema, hawezi kueleza chochote kuhusu mradi huo licha ya kuwa ulijengwa kwa usimamizi wa ofisi yake.

“Sina ‘comment’ kwa sababu waziri ameagiza na kama kuna wahandisi mizigo basi sheria ipo,” alisema.

Juzi, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alimwambia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick kuwa ili mradi huo unahitaji Sh6 bilioni.     
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge; Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Bibi Jenista Mhagama (Mb), akimsikiliza mkazi wa Tegeta, Basihaya Jijini Dar es Salaam, Jumanne Malongo alipokuwa akimueleza jinsi wembamba wa mtaro huo unavyosababisha maji kujaa katika makazi yao, jana wakati alipofanya ziara kuangalia jinsi wilaya hiyo ilivyojiandaa kukabili maafa ya Mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo, kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda.
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Manisipaa kinondoni, Ando Mwakunga akimueleza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge; Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Bibi Jenista Mhagama (Mb), uharibifu wa “kalvati” katika eneo la Boko, Ununio Jijini Dar es Salaam, jana wakati Waziri huyo alipofanya ziara kuangalia jinsi wilaya hiyo ilivyojiandaa kukabili maafa ya Mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo.

logoblog

Thanks for reading WAZIRI WA AJIRA JENISTA MHAGAMA AMFUKUZA KAZI MKANDARASI DAR......ATOA MASAA 6 KWA MKURUGENZI WA KINONDONI

Previous
« Prev Post