DOWNLOAD APP YETU HAPA

JINSI YA KUJUA KAMA MPENZI WAKO ANAKUPENDA KWA DHATI

  Eliafie Elifura      

HAKUNA kitu kinachowasumbua wengi katika uhusiano kama kutokuwa na uhakika na hisia za mwenza wako kwako. Wengi wamekuwa wakijaribu kwa hali na mali kutaka kujua kama kweli mwenza aliye naye anampenda au yuko naye kwa ajili ya tamaa na endapo akimaliza shida zake huenda ukamuacha.

Zipo njia nyingi unazoweza kuziangalia na kujua kama kweli mwenza uliye naye ana nia na upendo wa kweli kwako, njia hizo ni pamoja na kuangalia mienendo yake anapokua na wewe au mbali nawe.

Ukitaka kujua kama mwenza wako anakupenda na kukujali, lazima awe na kumbukumbu ya kile ulichokisema, hapa hasa kwa wanaume, hata kama mwenza wake amesema jambo lisilo na maana lakini kwa kuwa anampenda na kumjali hujitahidi kuwa makini na kumsikiliza na hivyo kuwa na kumbukumbu nzuri.

Aidha ili kujua kama mwenza wako ana hisia nzuri kwako, utaona namna anavyokuchukulia mkiwa pamoja, hujaribu kufanya yale yanayokupendeza na kamwe hatokubali uumie au upate taabu.

Jambo lingine ni pale anapokushirikisha katika mipango yake ya maisha, endapo mwenza wako atazungumzia ndoto zake za maisha ya baadaye bila kukuhusisha ujue kuwa uhusiano huo hauna hisia za upendo.

Mwenza anayekupenda katika mipango lazima akushirikishe ikiwa ni pamoja na kukujumuisha katika mipango hiyo.

 Aidha unaweza kutambua kama unapendwa au la na mwenza wako, pale mnapokua kwenye umati wa watu wengi wakiwemo rafiki zake, anapokua jirani na wewe, kukushika mkono na kutoona aibu ya kukutambulisha, ukiona hivyo tambua wazi kuwa hisia za mwenza wako kwako ni za kweli.

Dalili nyingine ni pale mwenza wako anapoanza kufuatilia nyendo zako na kuonesha wivu wa waziwazi kwako, kutokupendezwa pale anapokuona unazungumza kwa ukaribu na wanaume au wanawake wengine tofauti na wewe.

Wenza wengine wanaonesha upendo wao kwa kuhakikisha anajua kila kitu kuhusu maisha yako na kuwa tayari kusaidia pale panapoonekana panahitaji msaada na endapo mnagombana huwa tayari kumaliza ugomvi kwa njia nzuri ya maelewano na si kuwekeana visasi.

Aidha jambo lingine ni pale unapoona anajitahidi kwa hali na mali kufahamiana na ndugu zako lakini kikubwa akijitahidi sana ndugu zako hao wamkubali.

Ukweli ni kwamba zipo dalili nyingi zinazoweza kukusaidia kutambua kuwa uhusiano ulionao ni wa kudumu au la, jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa hata wewe mwenyewe unajitahidi kuwa chachu ya kuimarisha uhusiano wako na si kutegemea kila kitu kutoka kwa mwenza wako.
logoblog

Thanks for reading JINSI YA KUJUA KAMA MPENZI WAKO ANAKUPENDA KWA DHATI

Previous
« Prev Post