Katika maoni ya viongozi hao wa dini na wananchi, wako waliomkosoa huku wengine wakisema viongozi wa namna hiyo wanapaswa kuombewa.

Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, alisema mambo hayo si ya kiistarabu na yasiyofaa na kwamba yanapaswa kukemewa.

“Tunaamini alighadhibika lakini tukumbuke kuwa kiongozi wa dini ni binadamu si malaika, hivyo anapokosea naye anapaswa kuombewa ili asianguke tena," alisema Askofu Niwemugizi.

Aliongeza kuwa: "Leo anaweza kufanya vizuri kesho akakosea, ingekuwa mahubiri tunayotoa kila siku yanamaliza uovu duniani, basi mambo yangekuwa safi, lakini tunapaswa kuishi kwa kuombeana ili kujizuia kutofuata mihemko yetu.”

Taarifa zilizoifikia Nipashe Jumatano usiku kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilidai Mzee wa Upako alikamatwa baada ya kulalamikiwa kutoa lugha chafu kwa majirani zake na kufunga barabara ya umma.

Chanzo chetu ndani ya jeshi hilo kilidai kuwa Mzee wa Upako, Jumatano asubuhi alifika nje ya nyumba ya majirani zake wilayani Kinondoni, Dar es Salaam na kuanza kutoa lugha zisizofaa, akiwatuhumu kuwa wamekuwa wakimwita mlevi na hafai kuwa mchungaji.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum, alisema jambo lililofanywa na mchangaji huyo si zuri hasa kwa kiongozi kama yeye kwa sababu viongozi wa dini wana mafundisho ya namna ya kuishi.

“Anayefanya kinyume cha mafundisho atakuwa ameteleza kwa sababu yeye pia ni binadamu, tusidhani kama viongozi wa dini ni malaika kwa hiyo anatakiwa kujipima na kuomba radhi waumini na kanisa lake,” alisema.

Alisema kama kweli kiongozi huyo alifanya jambo hilo, ni muhimu akaungama na kukubali makosa kwa sababu alilofanya siyo jambo zuri.

Akata simu
Mchungaji Lusekelo alipopigiwa simu na gazeti hili jana, alipokea na kuitikia vizuri lakini punde baada ya mwandishi kujitambulisha, aliguna na kukata simu.

Alipoandikiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) ili atoe ufafanuzi juu ya nini kilichotokea na kama kweli alipishana kauli na majirani zake, hakujibu licha ya kuonyesha umepokewa.

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam iliyoahidi kuzungumzia jambo hilo jana, iliwaambia waandishi wa habari kuwa imeahirisha hadi keshokutwa.

Habari za tukio la Mzee wa Upako kukamatwa na polisi kwa tuhuma za kuwafanyia fujo majirani zake na kufunga barabara katikati ya wiki jijini Dar es Salaam, jana zilikuwa gumzo mitaani na kwenye mitandao ya kijamii pia.

Akizungumzia tukio hilo kwenye mtandao mmoja wa kijamii, Abel Pangamawe alisema Mzee wa Upako ni binadamu na ana dhambi kama wengine.

"Ameanguka anahitaji msaada. Aombewe ili arudi katika hali ya kawaida… ndiyo maana falsafa ya makanisa ya kale inasema tenda ninalokwambia usitende ninalotenda.

"Wahubiri wengi hawawezi kutufikisha mbinguni, tufuate maandiko kama roho mtakatifu atavyotuongoza si hawa binadamu," alisema.

Paul Moses alikumbusha kwa kuwa na yeye ni binadamu, tusimhukumu. "Ila namuamini sana... hata maombi yake yamenisaidia sana."

Christopher Buke alisema kwake mazingira ya kukamatwa kwa Lusekelo ni msiba mkubwa.

"Hii haina tofauti na kumuona baba yangu mzazi au mama yangu akiwa uchi, mwenyezi Mungu amsaidie mtumishi wake (Mzee wa Upako) na kumuinua tena".

Gladys Mwinuka alisema si kila atakayesema bwana bwana ataurithi ufalme wa Mungu.

"Mchungaji mchungaji, kama wewe unafanya haya itakuwaje unaowahubiria?" aliandika Deogratias Malamo.

Komanya Kitwala alisema Lusekelo ni mwanadamu kama wanadamu mwingine hivyo yeye pia hukosea.

"Inawezekana alirushiwa maneno ya kejeli ama dhihaka, sasa na yeye akahamaki," aliandika Kitwala.

"Hata sisi tunafanya makosa, lakini tusiwe wepesi wa kuhukumu. Watumishi wa Mungu wengi walifanya madhambi makubwa, akina Daudi, na bado walitubu na baraka zikawa juu yao sembuse huyu anayetishia kutokana na hasira? Tusihukumu."
Daudi Mlaule aliandika kuwa mkasa huo 'umemchosha' hivyo "Mungu pekee ndiye anayejua."

Adelta Paul aliandika kuwa alihisi kuchanganyikiwa kwa taarifa za matukio ya Mchungaji Lusekelo "maana tulivyokuwa tunampenda na kuangalia mahubiri yake, (ni) mpaka tunaongeza sauti kubwa kabisa."

"Halafu mtu tunaemtegemea kusikiliza mafunzo yake ili tujifunze tena yeye ndiyo anaharibu, jamani anapotea".

Peter Jaluo aliandika kuwa Rais John Magufuli alipomtembelea mapema mwaka huu alisema anafanya kazi nzuri ya kiroho, na kwamba hata yeye ni mhumini wake na atamtengenezea barabara ya kwenda kanisani kwake.
"Kama mambo yenyewe ndiyo haya basi tena," aliandika.

Rais Magufuli atembelea Kanisa la Maombezi Ubungo Kibangu Juni 5 ambapo aliahidi kutengeneza barabara ya kilomita moja ya Ubungo External inayofika kanisani hapo, ambayo ilikuwa imejaa mashimo.

Source: Nipashe
BOFYA LIKE KUUNGANA NASI FACEBOOK!


Je wewe una mtaji wa Ths.250,000/= au 510,000 au 1,020,000?..na unahitaji kufanya biashara kubwa kwa mtaji huo ufanikiwe?..basi kama ndiyo njoo tukuonyesha njia ya kutekeleza malengo yako...piga 0625 539 100 
Top