Msikie Huyu Mwalimu Muhimbili anasimulia anavyoishi na moyo wa betri | Masama Blog


Msikie Huyu Mwalimu Muhimbili anasimulia anavyoishi na moyo wa betri

Tokeo la picha la PACEMAKERUWEKAJI kifaa kitwacho 'Pacemakeri' au kupandikizwa betri katika moyo wa binadamu ulianza mwaka 1960 na hadi sasa, kuna jumla ya watu milioni tatu wenye matatizo hayo ya moyo na kuwekewa vifaa hivyo.
Prof. Gernard Msamanga

PROF MSAMANGA.

Takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka huu pekee kuna watu 600,000 duniani, kwa mujibu wa mtaalamu wa Upasuaji Moyo wa Watoto, Dk. Godwin Geoffrey wamewekewa vifaa hivvo, ambavyo kasi yake ni kuongeza uwezo wa moyo kutoa mapigo.

Mwanataaluma wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Prof. Gernard Msamanga, ni miongoni mwa waliowekewa kifaa hicho, tangu mwaka 2010.

Hiyo ni kutokana na badaa ya kugundulika kuwa moyo wake umetanuka au katika lugha ya kitaalamu inajulikana kama 'Idiopathic cardiomyopathy'.

Alipozungumza na Nipashe hivi karibuni kuhusu kifaa hicho alichowekewa, Profesa Msamanga anasema amekuwa akifanya shughuli zake kama kawaida, licha ya kuwa na mapungufu hayo ya kiafya.

"Ninaweza kufundisha hata kwa zaidi ya saa nane nikiwa darasani na wanafunzi wangu uzuri wake wanafahamu. Siku moja nilipatwa na tatizo nikiwa chuoni," anasema Prof. Msamanga.

Anasimulia kwamba hilo lilimtokea wakati akiteremka ngazi chuoni na ndipo baadhi ya wanafunzi walimchukua na kumpeleka katika eneo lililo na hewa zaidi.

"Walinisaidia wakanipeleka eneo lenye hewa safi, wakanilegeza tai ili nipumue vizuri. Baada ya hapo nilipata nguvu na kuendelea na shughuli zangu kama kawaida," anasema.

Anasema kabla ya kufanyiwa upasuaji huo, alikuwa akipata mshituko wa moyo mara kwa mara, tofauti na alivyo sasa.

MASHARTI YA AFYA


Prof. Msamanga anasema masharti aliyopewa tangu alipofanyiwa upasuaji, ni pamoja na kutotumia vitu vya sumaku, asinywe maji mengi kupita kiasi na amekuwa akitekeleza masharti hayo.

"Sitakiwi kuweka sumaku jirani na kifua changu. Mfano, kuvaa beji iliyo na jina kukutambulisha taasisi unayofanya kazi inayokaa kifuani upande wa kushoto siruhusiwi kuvaa," anaongeza.

"Airport (Kiwanja cha ndege) sikaguliwi na mitambo yeyote. Nina kitambulisho maalumu ambacho natumia mahali popote, nikisafiri hata nje ya nchi," anasema.

Anaongeza kwamba, anatumia simu huzingatia pale inapoita na hapokei kupitia sikio la kushoto na badala yake anatumia sikio la kulia.

Prof. Msamanga anasema masharti mengine aliyo nayo ni kwamba, mara zote anazunguka akiwa na dawa zake na kila siku anatumia vidonge vinne na maji kiasi cha lita moja na nusu kwa siku.

MKURUGENZI JKCI

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, JKCI, Prof. Mohamed Janabi, anasema wagonjwa waliowekewa kifaa hicho huishi kwa masharti.

Anataja masharti hayo kuwa ni pamoja na kutumia dawa kwa kuzingatia ushauri, kutopita maeneo yenye sumaku na mionzi.

Profesa Janabi anasema kuwa, mgonjwa aliyewekewa kifaa hicho ana maisha ya kiafya yanayofanana na wagonjwa wengine wasio na matatizo hayo.

Anasema, hivyo wanapougua maradhi mengine wanapaswa kupatiwa matibabu kama wengineo, ingawa wanahitaji ushauri na uangalizi wa karibu.

Kwa mujibu wa Prof. Janabi, wagonjwa wanaowejezwa kifaa hicho, wanapopelekwa nje ya nchi kuwekewa kifaa hicho huwagharimu Sh. milioni 120, ilhali katika taasisi ya JKCI ni Sh. milioni 8.5 tu kwa wagonjwa walio na bima ya afya na wasiokuwa na bima ni Sh. milioni 40.

DAKTARI AELEZA


Mtaalamu wa Upasuaji Moyo wa Watoto wa JKCI, Dk. Godwin Geoffrey, anasema kwa kawaida mapigo ya moyo ya binadamu ni kati ya 60 hadi 100 kwa dakika na inapotokea kuwa chini ya hapo, hujikuta anapoteza fahamu kila mara.

Anatoa mfano, mapigo ya moyo ya mgonjwa mtoto mwenye miaka sita,aliyewahi kumtibu katika taasisi anayofanyia kazi, kabla ya kuwekewa kifaa hicho, yalikuwa ni kati ya miaka 20 hadi 25 kwa dakika moja.

Anasema hali hiyo taratibu ya moyo, ambayo ni kasi hafifu ndiyo yali husababisha kupoteza fahamu, kwa kuwa moyo unavyosukuma damu kwenda mbele haiendani na mapigo ya moyo.

CHANZO CHAKE


Dk. Geoffrey anasema walio tatizo la anachokiita kitaalamu kama 'heart block' au mfumo wa umeme katika moyo kutokuwa sawa, hutokana na sababu nyingi.

Anazitaja kuwa baadhi ya watu huzaliwa wakiwa na hali hiyo.

Kwa mujibu wa Dk. Geoffrey, maradhi hayo huanza tumboni mwa mwa mama pale yanapovuka katika kondo la mtoto, hata kumhamishia maradhi hayo.

Ni hali inayotokea kwa kuingia katika mfumo wa damu wa mtoto na ndipo anapohamishiwa maradhi.

Dk. Geoffrey anasema kuwa, asilimia 70 ya watoto wanaokumbwa na tatizo hilo, hufia tumboni, huku asilimia 25 ni wa kuzaliwa.

Anaeleza kuwa, watoto wanaopatwa na tatizo hilo wakiwa tumboni na ndio aina ya tatizo alilokuwa nalo mtoto aliyewekewa moyo wa betri kupitia JKCI.

Dk. Geofrey anarejea takwimu za kitaifa, kuwa ni tatizo linalomkabili mtoto mmoja, kati 22,000 wanaozaliwa nchini.

"Ilikuwa ni ajabu kwetu na bahati kwa mtoto ambaye ana 'heart block' na akagundulika. Kwa taasisi hii, ni wa kwanza kugundulika, kwa kuwa wengi wao hupoteza maisha tangu wakiwa tumboni", anasema.

Mtaalamu huyo anasema kuwa, kuna watu wazima wenye tatizo la 'heart block' ambao sababu zao zinatokana na mambo mengine tofauti, kama vile maradhi kutokana na umri mkubwa.

Pia anasema maradhi kama kisukari, shinikizo la juu la damu kwa watu wazima huwa ni sababu mojawapo ya mtu kupatwa na hali hiyo.

Tabibu Dk. Geofrey, anasema duniani kuna watu maarufu wengi waliowekewa kifaa hicho na kiwawezesha kufanya shughuli zao kama kawaida.

Anafafanua; "Aliyekuwa Kocha wa timu ya Manchester United (Ya Uingereza), Sir Alex Ferguson, anaishi na kifaa hicho kwa miaka 10 sasa.

"Mwanamuziki maarufu, Sir Elton John na Dick Chen, aliyekuwa Naibu Rais wa Marekani, katika uongozi wa Rais George Bush."


PACEMAKER NI NINI?


Wataalamu wa masuala ya moyo, wanasema upasuaji wa moyo uliofanyika na watu kuwekewa kuweka kifaa cha bandia ndani ya moyo, huitwa Pacemaker.

Inaelezwa, moyo wa binadamu umeundwa na kitu kinachoitwa Sinotrial Node, ambacho kazi ya kuzalisha nishati kama ya umeme, ili kusaidia moyo kusukuma damu vizuri kwa mapigo yanayotakiwa kwenye mwili.

Sinoatrial ipo katika sehemu ya juu ya kulia ya moyo wa binadamu.

Namna 'betri ya moyo' inavyofanya kazi ni kwamba, Iwapo 'pacemaker' ya asili katika moyo wa binadamu inashindwa kufanya kazi,
ndipo 'pacemaker' ya kutengenezwa iliyopandikizwa katika moyo wa mwanadamu husaidia kufanya kazi hiyo.

Kifaa hicho huzalisha umeme, unaosaidia kusukuma damu na hufanya kazi katika kiwango sawa sawa na ile ya asili.

Hicho ni kifaa kilichoundwa na betri zinazoweza kubadilishwa kila baada ya miaka ama mitano au sita, na kwamba mtu mwenye kifaa hicho mapigo ya moyo husikika kama mishale ya saa za ukutani.

BOFYA LIKE KUUNGANA NASI FACEBOOK!


UNAIJUA BIASHARA YA FOREVER LIVING?....Kama una mtaji kuanzia 250,000 hadi 1,020,000 na unapenda kujikwamua na kubadilisha maisha yako kupitia biashara hii Tupigie simu nambari 0625539100 au 0625539200