Ticker

10/recent/ticker-posts

Mjue mpenzi mkorofi kwa hizi tabia zake

young-couple-arguing-on-a-sofa-136381366849303901-130702114836NAAM ni siku nyingine tena tumekutana katika kona yetu hii ya Sindano za Mahaba. Kwa wale wazima kama mimi ni jambo la kumshukuru Mungu.
Hivi unamjua mpenzi mkorofi yupoje? Kama wewe ni mwanamke mada hii itakusaidia sana kumjua mpenzi mkorofi kwani wengi wanaingia katika uhusiano wa kuishi pamoja lakini wakishaingia mitafaruku inakuwa mingi.
Wengine wamekuwa vipofu katika kuona baadhi ya dalili mbaya zinazoonekana katika hatua za mwanzoni katika uhusiano na mara wanapoendelea mbele na kufanya maamuzi mazito hususan maamuzi ya kuamua kuoana au kuishi pamoja, mabadiliko makubwa yanaanza kutokea na hali inaanza kuleta misuguano mingi na maumivu mengi.
Nitakuonesha dalili ambazo unaweza kuziepuka mara baada ya kuona mpenzi/mume wako anakufanyia haya pia dalili hizi zitakusaidia zaidi kuwafahamu wanaume.
Kwa nini wanawake?
Wanawake wengi wamekuwa wakiumizwa zaidi na kukatishwa tamaa na mabadiliko ya tabia za wanaume mara wanapozama katika dimbwi la mapenzi. Ingawa pia wapo pia wanaume wanaoumizwa kutokana na mabadiliko ya tabia za wapenzi wao na wao siyo mbaya wanaweza pia kuzitazama dalili hizi.
WIVU
Mpenzi wako anakuwa na wivu sana kwa ule muda unaotumia kuwa na wafanyakazi wenzako, marafiki na hata ndugu zako, ingawa siyo kwamba anataka muda huo awe na wewe.
Anakuwa na tabia za kukuudhi na kukutawala, ataangalia sana kutoka na kuingia kwako, nyendo zako na hata matumizi yako ya fedha na kama ukimuuliza kwa nini anafanya hivyo, atajitetea kuwa anakusaidia kufanya maamuzi sahihi.
Taratibu anakutenga na wote walio karibu na wewe. Pia anajaribu kukutenga na wale wanao-onekana kuwa msaada kwako kama vile, wale unao-wasiliana nao kwa simu, wafanyakazi wenzako na hata ndugu zako wa karibu.
LAWAMA
Huwa na tabia ya kuwalaumu sana wengine kwa matatizo anayo-yapata. Mfano anapo-kosa kazi, anapo-shindwa shuleni nk. Kila kitu ni kosa la mtu mwingine na siyo yeye.
Huka-sirishwa na kuudhiwa na vitu vidogo-vidogo na vya kawaida katika maisha ya kila siku, mfano akiambiwa afanye kazi zaidi ya muda wa ofisi, akiombwa amwangalie mtoto, anapopingwa katika kitu kidogo nk.
MKATILI
Anakuwa na tabia za kikatili kwa wanyama (wafugwao) na hata kwa watoto. Haumizwi pale anapoona maumivu au kuteseka kwa wanyama au watoto.
Ni wenye tabia ya mabavu hususan katika tendo la ndoa, hawatajali hisia zako, umelala usingizini au unaumwa, bali hujali zaidi kuzitimiza haja zao.
Ni wenye maneno makali ya kuumiza na ya kushusha hadhi, huweza kukuamsha usingizini ili akutukane au kukugombeza. Akianza malumbano hakupi upenyo wa kwenda kulala, anaweza kulalama usiku mzima.
HATABIRIKI
Siyo watu wakutabirika, ni watu wenye hisia za kubadilikabadilika, mara muda huu ana furaha na kuonesha mapenzi, mara ghafla anakasirika na kutaka kuadhibu mtu.
Anaweza akawa na historia ya tabia za kikorofi na kigomvi, labda amewahi kuwa na matukio ya kuwapiga marafiki zake, akijitetea kuwa alipitiwa tu na hasira.
Ni mwenye vitisho na tabia za kuashiria fujo, mfano kupenda kutishia akisema; ‘Nitakuzaba vibao’, ‘Nitakuua’, ‘Nitakuvunja shingo’,  ‘Nitakufanyia kitu mbaya’ ‘Achana na mimi’ n.k.
Mwenye tabia ya kupiga au kugonga vitu kwa hasira, kuvunja vitu vyako, kukurushia vitu wewe au watoto kwa hasira.
Hutumia nguvu anaposisitiza hoja yake, mfano kukushika nguo au kukukandamiza ukutani na mara nyingine kukusukuma.
Kwa leo niishie hapa. Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.