Ticker

10/recent/ticker-posts

Chunga Tabia zako za asili ‘zitakukosti’ kwenye mapenzi!

vegeterians-couple-bedMPENZI msomaji wa XXLove tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha kwa mara nyingine Jumatatu hii murua, tukiwa wenye siha tele. Tunasema ahsante Mungu!
Wiki iliyopita nilizungumzia suala la mtu kutokuwa na fedha lakini pia kutokuwa na uwezo mzuri kwenye suala la mapenzi. Huna fedha, sawa, lakini hata mapenzi nayo yanakushinda? Nimepokea simu na sms nyingi kuhusu mada hiyo ndipo ikaibuka mada ya leo ambapo mmoja wa wasomaji, yeye alizungumzia suala la tabia za asili za wapenzi namna ambavyo zinaweza ‘zikawakosti’ kwenye suala zima la mapenzi na uhusiano, nami nikaona yafaa na wewe ukalijua hilo.
Kama mwenza wako ana tabia ya asili yoyote ile unayoihisi au kuifahamu, inakupasa kuwa makini naye kwani tabia hiyo au hizo zinaweza kukuathiri kisaikolojia au kimazingira.
Inaweza kukuathiri kisaikolojia kwa maana ni tabia ambayo ni ngumu kuiondoa katika damu ya mtu ambaye amezaliwa na tabia hiyo, hivyo itakulazimu kutumia muda mwingi katika kutafuta njia mbadala ya tabia asili ya mwenza wako.
Yawezekana ikawa ni vigumu kufahamu ni kwa namna gani unaweza kulizoea tatizo lake na kuishi naye katika uhusiano wa kimapenzi. Ila kama ulimpenda kwa dhati na hukulazimishwa kuwa naye, basi jifunze kumzoea
 na kuepuke baadhi ya tabia hizo.
Kwa upande wa kimazingira, tabia ya asili inawezekana kuwa ni mwenza wako kuwa mkorofi, mmbeya, malaya na kadhalika, jambo ambalo laweza kukugombanisha na wazazi, ndugu, majirani na hata marafiki zako, kwani kila kukicha kesi za ugomvi mtaani zitamhusu mkeo au mmeo, mara kapigana na fulani, katukanwa na fulani au unahisi katembea na Kulwa au Zulfa wa nyumba ya pili.
Kiukweli tabia za asili ni ngumu kuzizoea au kuziishi ila kwa kuwa umeshaamua kuwa mwili mmoja, huna budi kukubaliana na tabia hizo ili maisha yasonge.
Kwa ushauri wangu, ni vyema vijana wa sasa wakawa wazi katika maisha ya uchumba na kuishi maisha halisi na kwa muda, tena mkiwa karibu. Hii itasaidia kuzifahamu baadhi ya tabia za asili za umpendaye.
Kwa kuzifahamu, itakusaidia kufahamu ni kwa namna gani utaishi naye na kama ikitokea akakukwaza, basi utajua ni kwa namna gani utamvumilia au kumtuliza na maisha yakaendelea.
Uhalisia wa maisha ni eneo muhimu mno katika uhusiano. Kama kweli ni muungwana, jiachie, acha kujifanya ni mstaarabu ilihali wewe siyo mstaarabu, acha kujifanya unawapenda ndugu wa mwenza wako wakati moyoni unawachukia. Huo ni unafiki na ni maisha ya kuigiza ambayo ipo siku yatakushinda.
Ni hayo tu kwa wiki hii lakini usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mitandao ya Kijamii ya Facebook, Instagram: mimi_na_uhusiano au jiunge na Group la M&U kwenye WhatsApp kwa namba hiyo hapo juuu.