Ticker

10/recent/ticker-posts

Shuhudia Rais Magufuli Alivyoagana Na Kiongozi Mkuu Wa Bohora Duniani, Ikulu Jijini Dar

Jumuiya ya Madhehebu ya Dawoodi Bohra imetoa mchango wa Dola za Marekani laki mbili na nusu (Usd. 250,000) sawa na Shilingi Milioni Mia Tano Arobaini na Tano za Kitanzania (Ths. 545,000,000) kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea katika Mkoa wa Kagera tarehe 10 Septemba, 2016.

Kiongozi Mkuu  wa Madhehebu ya Bohra Duniani Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin amekabidhi mchango huo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, jana walipokutana na kufanya Mazungumzo leo tarehe 13 Oktoba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kati ya fedha hizo Dola za Marekani laki moja (Usd. 100,000) zimetolewa na Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin mwenyewe, Dola za Marekani laki moja (Usd. 100,000) zimetolewa na Viongozi wengine wa Madhehebu ya Bohra na Dola za Marekani Elfu Hamsini (Usd. 50,000) zimetolewa na wana Jumuiya ya Bohra wa Tanzania.

Pamoja na kutoa mchango huo, Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin ameahidi kuwa Jumuiya hiyo ambayo inamiliki hospitali kubwa zilizopo maeneo mbalimbali duniani ikiwemo India, itajenga hospitali hapa nchini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu.

Pia Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin ameahidi kuwa Jumuiya ya Bohra itatoa udhamini wa masomo ya udaktari kwa vijana wa Tanzania na pia itadhamini matibabu kwa wagonjwa 20 watakaopelekwa nchini India kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Kwa Upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemshukuru Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin na Jumuiya nzima ya Dawoodi Bohra kwa mchango walioutoa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera na pia kwa kufanyia mkutano wao wa mwaka hapa nchini uliowaleta wageni takribani 31,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin nakushukuru sana kwa kuja hapa nchini kwetu na kutuletea mkutano huu mkubwa, ujio wenu umeimarisha uhusiano kati ya Bohra na Tanzania na pia umechangia uchumi wa nchi yetu.

“Nakushukuru pia kwa nia yenu ya kujenga hospitali hapa nchini, kuwasomesha madaktari na kudhamini matibabu ya wagonjwa huko India, naomba nikuhakikishie kuwa mchango mlioutoa utatusaidia sana na pia mkijenga hospitali na kufundisha madaktari mtakuwa mmesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo Serikali ingetumia” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewaalika wanajumuiya ya Dawoodi Bohra kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, kilimo, usafirishaji, madini na uvuvi na amewahakikishia kuwa Serikali itawaunga mkono wote watakaokuwa tayari kuja kuwekeza Tanzania.

Jumuiya ya Madhehebu ya Dawoodi Bohra Duniani imeadhimisha mwaka mpya wa Kiislam na kumbukumbu ya kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W) aitwaye Imamu Hussein ambapo maadhimisho yake ya kidunia yaliyoambatana na tamasha la zaidi ya wiki mbili yamefanyika hapa nchini kuanzia tarehe 01 Oktoba, 2016 hadi tarehe 11 Oktoba, 2016.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
13 Oktoba, 2016