Ticker

10/recent/ticker-posts

SIFA 8 KUBWA ZA MWANAMKE AMBAYE NI ‘WIFE MATERIAL’!

Kuoa/kuolewa ni jambo muhimu sana katika maisha ya kila binadamu. Ndiyo maana inaelezwa kuwa, matukio makubwa muhimu katika maisha ya kila mtu ni kuzaliwa, ndoa na kufa!Kutokana na ukweli huo, vijana wengi wamekuwa wakitamani kuoa na kuolewa lakini utafiti mdogo nilioufanya unaonesha kwamba, wasichana wengi wamekuwa wakiitamani ile heshima ya kuolewa.

Hawataki kuwa viruka njia, wanataka waipate ile raha ya ndoa, raha ya kuitwa mke wa mtu lakini pia wengine wanataka waingie kwenye ndoa ili wazae.Kimsingi kuna utitiri wa wanawake wanaotaka kuolewa huko mtaani lakini wanaume wengi ambao wako kwenye umri wa kuoa wanadai bado wapo wapo kwanza.
Wanasema wanawake wa kuoa hawajawaona, wanahisi wakiingia kwenye ndoa wataumizwa eti kwa sababu usanii umekuwa ni mwingi kwenye mapenzi.Hata hivyo, wapo wanaume wengi ambao wanahangaika kutafuta wachumba. Si kwamba wasichana wa kuoa hawapo, wapo lakini tatizo ni kumpata yule mwenye vigezo vya kuitwa mke ‘wife material’. Sasa, leo nataka kuwapa msaada wanaume ambao wanahangaika huku na kule kumbaini mwanamke mwenye sifa ya kuitwa mke.

ANGALIZO
Kuna wanawake ambao ni wajanja sana, wanaweza kujivisha ngozi ya mbuzi kumbe ndani ni chui. Wana uwezo mkubwa sana wa kuficha makucha yao lakini wakiingia kwenye ndoa utashangaa namna watakavyoyatoa na kukufanya ujute.
Kwa maana hiyo basi, kama unatafuta mke kwa maana halisi ya mke, unatakiwa kutumia muda mrefu sana kumchunguza huyo ambaye unahisi anaweza kuwa mama wa watoto wako.

SIFA ZA MWANAMKE ‘WIFE MATERIAL’
Anayejua kuna shida na raha
Wapo wanawake ambao wao wanajua kila siku ni Ijumaa, yaani hawatambui kwamba kuna Jumamosi na Jumapili pia. Watu hawa ni wale wanaodhani maisha ni raha tupu na kwamba wanaoishi kwenye shida ni wajinga.Ukweli hauko hivyo, maisha yana changamoto nyingi sana. Kuna siku mambo yanaweza kuwa si mazuri lakini siku nyingine mambo yakawa supa. Mwanamke wa kuoa lazima ajue hivyo.

Hana tamaa za pesa
Katika maisha ya sasa mwanamke anayependa sana pesa ukikubali awe mkeo mtasumbuana sana. Kwa maana hiyo mwanamke ambaye utagundua hana tamaa ya pesa, kwamba ikiwepo, ikikosekana anabaki kuwa yeye, huyu ni ‘wife material’.

Hayuko tayari kukuona huna amani
Mwanamke ambaye unaona kabisa unapokuwa na matatizo anaumia, anahaha kuhakikisha anakurudisha kwenye hali ya kawaida, huyo anafaa kuwa mkeo.

Anapenda watoto
Utajuaje kama ana mapenzi na watoto? Iko hivi; katika uhusiano wenu ukiona ni mtu wa kupendapenda sana watoto wa marafiki zake, kuwanunulia zawadi, kuwashauri wenzake namna nzuri ya kuwalea watoto, hata akija kupata wa kwake itakuwa ni hivyohivyo.

Heshima kwa kila mtu
Msichana ambaye anaheshimu kila mtu, mdogo na mkubwa, anawapenda na kuwaheshimu ndugu, jamaa na marafiki zako, huyu ana sifa ya kuwa mkeo pia.

Anajishusha
Ogopa sana mwanamke ambaye anataka usawa. Anayekufaa ni yule anayejua yeye ni mke, na wewe ni mume. Anayetambua kuwa, mwanaume ndiye kiongozi wa familia.

Anakuongoza kwenye mema
Kama mpenzi wako ni wa kukutaka kila siku muende baa au mfanye madili hatari ili mpate pesa, huyu hana sifa ya kuwa mkeo. Mke ni yule ambaye atakuongoza kwenye kutenda mema na kuacha mabaya.
Kwa mfano kama unakunywa pombe atakushauri uache, kama siyo mtu wa ibada, atakushawishi umjue Mungu wako na mambo mengine kama hayo.

Anajua maisha na mapenzi
Mapenzi yanachukua sehemu kubwa ya maisha ya binadamu. Kwa maana hiyo mwanamke anayekufaa wewe ni yule ambaye anayajua mapenzi vilivyo lakini pia anajua maisha. Kama yeye ni mtaalam wa majamboz tu lakini linapokuja suala la mambo ya kimaendeleo hayumo, huyo hafai. Pia akiwa yeye ni mtu wa mambo ya kimaendeleo tu lakini linapokuja suala la mapenzi ni sifuri, pia hakufai.